Home Kitaifa UCSAF YAKAMILISHA UJENZI WA MINARA 2,199 YA MAWASILIANO NCHINI

UCSAF YAKAMILISHA UJENZI WA MINARA 2,199 YA MAWASILIANO NCHINI

Celebrating 25 Years of NHIF

Na Magrethy Katengu— Mzawa media
Dar es Salaam

Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) umefanikiwa kujenga minara 2,199 kati ya minara 2,324 iliyopangwa kujengwa katika awamu mbalimbali, hatua inayolenga kupanua upatikanaji wa huduma za mawasiliano na kupunguza changamoto ya mawasiliano katika maeneo ya vijijini na mijini nchini.

FAHARI AFYA

Akizungumza na wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Novemba 3, 2026, katika kikao kazi kilichoratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, Mkurugenzi wa Utafiti na Maendeleo wa UCSAF, Albert Richard, amesema miradi hiyo imetekelezwa katika mikoa 31 ya Tanzania Bara na Zanzibar, ambapo kata 2,053 kati ya 2,306 zilizolengwa tayari zimefikiwa na huduma za mawasiliano.

Amesema katika mradi wa ujenzi wa minara 758, yote imekamilika na kuwashwa, ikiwa ni sehemu ya uwekezaji wa Sh bilioni 126 unaolenga kuboresha huduma za mawasiliano kwa wananchi wapatao milioni 8.5 katika kata 713 na vijiji 1,401.

Richard amesema mradi huo umetekelezwa kwa ushirikiano na kampuni za simu za Airtel, Viettel, Yas, TTCL na Vodacom.

Aidha, amesema Serikali kupitia UCSAF inaendelea kutekeleza mradi wa awamu ya 10 unaohusisha ujenzi wa minara 287 katika kata 287, ambapo hadi sasa minara 65 imewashwa, sawa na asilimia 23 ya utekelezaji. Mradi huo wenye thamani ya Sh bilioni 29 ulizinduliwa Desemba 5, 2025 na unatarajiwa kukamilika ndani ya miezi 15.

Katika sekta ya utangazaji, amesema UCSAF imefadhili ujenzi wa vituo 11 vya kurushia matangazo ya Redio ya Taifa (TBC), ambavyo tayari vimekamilika kwa gharama ya Sh bilioni 2.5, huku vituo vingine 26 vikiwa katika hatua mbalimbali za utekelezaji.

Kwa upande wa sekta ya elimu, Richard amesema shule za umma 1,167 zimenufaika na mradi wa kupeleka vifaa vya TEHAMA na ujenzi wa maabara, ambapo Serikali imewekeza Sh bilioni 17.7 hadi Oktoba 2026.

Ameongeza kuwa mfuko huo umepeleka vifaa vya TEHAMA katika shule 22 zinazotoa elimu kwa wanafunzi wenye mahitaji maalumu, ikiwa ni hatua ya kuimarisha usawa na ujumuishi katika upatikanaji wa elimu ya kidijitali.
Katika kuimarisha matumizi ya teknolojia kwa walimu, amesema UCSAF imefadhili mafunzo ya TEHAMA kwa walimu 5,094 wa shule za msingi na sekondari za umma Tanzania Bara na Zanzibar tangu mwaka wa fedha 2016/17.

Amesema kwa mwaka wa fedha 2026/27, walimu wengine 692 wanatarajiwa kupata mafunzo hayo, wakiwemo walimu 100 wenye mahitaji maalumu.

Kuhusu huduma za posta, Richard amesema UCSAF imeendelea kuunga mkono juhudi za kuboresha huduma za Shirika la Posta Tanzania kwa kutoa vifaa vya kisasa vinavyorahisisha utoaji wa huduma.

Ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2024/25, mfuko huo ulitoa vifaa 50 vya Personal Assistance Devices (PDA), kompyuta 30, kompyuta mpakato saba, vifaa vya umeme vya UPS 30 na mashine tano kubwa za kunakili nyaraka.

Amesema katika mwaka wa fedha 2025/26, UCSAF ilipanga kuendelea kuimarisha huduma hizo kwa kutoa vifaa vingine, vikiwemo PDA 50, printa tano za matumizi ya viwandani, kompyuta za mezani saba, kompyuta mpakato saba, UPS tano na mashine nne za kunakili nyaraka.

Katika hatua nyingine, amesema mfuko huo umeanzisha vituo vya intaneti ya bure katika maeneo yenye mikusanyiko ya wananchi, yakiwemo Viwanja vya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba jijini Dar es Salaam, Nyerere Square jijini Dodoma, Soko la Nyamagana mkoani Mwanza na Soko la Tabora ili kuwawezesha wananchi kupata huduma za kidijitali kwa urahisi.

Vilevile, UCSAF inaendelea na mpango wa kuunganisha ofisi za halmashauri na mkongo wa mawasiliano wa nyuzi za optiki (faiba), kwa lengo la kuboresha upatikanaji wa intaneti ya uhakika katika utoaji wa huduma za umma. Hadi sasa, maeneo 10 yamefanyiwa utambuzi huku mchakato wa manunuzi ukiendelea ili kumpata mkandarasi wa kutekeleza mradi huo.

Richard amesema UCSAF itaendelea kushirikiana na Wizara ya Mawasiliano na Teknolojia ya Habari pamoja na wadau mbalimbali wa sekta hiyo kuhakikisha huduma za mawasiliano zinawafikia wananchi wote, hususan wanaoishi katika maeneo yasiyo na mvuto mkubwa wa kibiashara.

Amesisitiza kuwa juhudi hizo ni sehemu ya mkakati wa Serikali wa kupunguza pengo la kidijitali na kupanua fursa za wananchi kutumia teknolojia katika elimu, biashara na shughuli nyingine za kiuchumi, sambamba na kuchochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!