
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Deogratius Ndejembi, amewataka Viongozi kuuenzi urithi wa aliyewahi kuwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Samuel John Sitta kwa kuishi misingi ya uadilifu, uwajibikaji na kujenga Taasisi imara.
Makamu wa Rais ametia ujumbe huo Novemba 3, 2026, katika Ukumbi wa Bunge jijini Dodoma, alipomwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwenye kumbukizi ya miaka 10 ya kifo cha Samuel John Sitta na uzinduzi wa kitabu kinachoelezea maisha na safari yake ya uongozi.
Makamu wa Rais amesema Hayati Samuel Sitta anakumbukwa kwa kutanguliza maslahi ya Taifa, kulinda hadhi ya Bunge na kusimamia heshima kwa taratibu na kanuni. Amesisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuyatafsiri mafunzo hayo katika utendaji wao wa kila siku.
“Uongozi wa kweli si njia ya kujitafutia umaarufu, hadhi au manufaa binafsi bali ni wajibu, utumishi, na ni kujitoa kwa ajili ya wengine,” amesema.
Aidha, amewahimiza Watanzania, hususan viongozi, vijana na wanafunzi, kukisoma kitabu hicho chenye kurasa 217 ili kujifunza kuhusu utumishi wa umma, uzalendo na umuhimu wa Taasisi imara katika kulijenga Taifa.
“Taifa linalokumbuka wajenzi wake huhifadhi utambulisho wake; Taifa linaloheshimu utumishi huwahamasisha wengine kutumikia; na, Taifa linalohifadhi historia yake hulinda mustakabali wake” amesema Makamu wa Rais.
Kwa upande wake, Spika wa Bunge, Mhe. Mussa Azan Zungu, amesema Sitta ataendelea kukumbukwa kwa uchapakazi, uzalendo na mchango wake katika Bunge na Taifa kwa ujumla. Kwa upande wake Mjane wa Hayati Sitta, Mhe. Margaret Sitta, amemwelezea kuwa mpenda haki aliyethamini ubunifu, uwajibikaji na falsafa ya “viwango na kazi.”
Hafla hiyo imewakutanisha viongozi mbalimbali, familia na watu waliowahi kufanya kazi na Sitta, huku ujumbe mkuu ukiwa kuendeleza urithi wake kwa vitendo na kutanguliza maslahi ya wananchi.









