Home Kitaifa TFS YAWAELIMISHA WAFANYABIASHARA WA MAZAO YA MISITU

TFS YAWAELIMISHA WAFANYABIASHARA WA MAZAO YA MISITU

WAKALA wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS) wametoa elimu kwa wafanyabiashara na wachongaji wa vinyago katika eneo la Mwenge jijini Dar es Salaam kuhusu sheria, kanuni na taratibu za uvunaji, usafirishaji na biashara ya mazao ya misitu, ikiwemo taratibu za kusafirisha bidhaa hizo nje ya nchi.

Akizungumza wakati wa utoaji wa elimu hiyo leo Agosti 12, 2026 Jijini Dar es Salaam, Mhifadhi wa Misitu wa TFS Wilaya za Kinondoni na Ubungo, Dotto Ndumbikwa, amesema hatua hiyo inalenga kuwawezesha wafanyabiashara kuelewa taratibu zinazotakiwa kufuatwa ili kufanya biashara zao kwa ufanisi na kuepuka usumbufu unaoweza kujitokeza kutokana na kutofuata sheria.

Amesema TFS imeambatana na wahifadhi kutoka Kanda ya Mashariki, wakiwemo wanaosimamia shughuli za misitu katika eneo la Uwanja wa Ndege, kwa lengo la kusikiliza changamoto zinazowakabili wafanyabiashara na kuzitafutia ufumbuzi.

“Tunapokaa kuwasikiliza na kuwapa elimu, inawasaidia wao kuendelea na biashara zao vizuri bila kupata matatizo,” amesema Ndumbikwa.

Aidha, amewataka wafanyabiashara wa mazao ya misitu kuhakikisha kabla ya kuanza biashara wanafika katika ofisi husika za Serikali kupata elimu kuhusu taratibu, vibali na tozo zinazohitajika ili biashara zao zifanyike kwa mujibu wa sheria.

Ndumbikwa pia amewataka wafanyabiashara kuwa makini wakati wa ukaguzi wa bidhaa zao, hususan katika maeneo ya viwanja vya ndege, kwa kuhakikisha anayefanya ukaguzi anajitambulisha na kuonyesha kitambulisho cha kazi.

Amesema wafanyabiashara wanapaswa kumtambua afisa mwenye dhamana ya kusimamia mazao ya misitu katika eneo husika ili kuepuka kukaguliwa na watu wasiohusika na kazi hiyo.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wasanii Wachongaji Tanzania (CHAWASAWATA), Sebastian Daniel Mbebe, amesema elimu hiyo imewasaidia wachongaji kuelewa vizuri sheria na taratibu ambazo awali zilikuwa chanzo cha malalamiko na changamoto katika shughuli zao.

Mbebe amesema moja ya changamoto iliyokuwa ikiwakabili wachongaji ni bidhaa za sanaa kuchukuliwa kama magogo hata baada ya kuwa zimechakatwa na kuwa bidhaa za sanaa.

Amesema kupitia elimu hiyo, wameelewa maeneo ambayo wao wenyewe walikuwa hawafuati taratibu ipasavyo, ikiwemo kutokuwa na baadhi ya vibali vinavyotakiwa kwa mujibu wa sheria.

“Hata sisi upande wetu kama uchongaji tulikuwa na makosa. Kuna vibali vingi tulikuwa hatuvitekelezi kwa mujibu wa sheria inavyotakiwa, lakini leo tumepata elimu na tumejua tunachotakiwa kufanya,” amesema Mbebe.

Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto ya tozo ambazo wanaziona kuwa ni kubwa na zinaweza kuwaathiri moja kwa moja wafanyabiashara na wasanii wanaotengeneza bidhaa za sanaa kwa ajili ya soko la ndani na nje ya nchi.

Ameeleza kuwa baadhi ya vinyago kama twiga, faru, simba na tembo vina uzito mkubwa licha ya kuwa tayari ni bidhaa zilizochongwa na kutengenezwa kwa ajili ya matumizi ya sanaa.

Amesema changamoto hiyo hujitokeza zaidi wakati mteja anaposafiri na bidhaa hizo kupitia uwanja wa ndege, ambapo anaweza kukutana na gharama za ziada zinazohusiana na uzito wa bidhaa.

Mbebe amesema wataendelea kufuata taratibu na kulipia vibali vinavyohitajika wakati wakisubiri hatua zaidi kuhusu mapitio ya tozo hizo.

Naye mdau wa mazao ya misitu, Mwanne Mashugu, ameishukuru TFS kwa kufika katika eneo lao la biashara na kutoa elimu ambayo amesema imewasaidia kuelewa taratibu za biashara kuanzia hatua ya kupata mazao hadi kuyafikisha madukani.

Amesema wamepata uelewa kuhusu namna ya kulipia tozo na vibali, ikiwemo vibali vya kusafirisha bidhaa, jambo litakalowasaidia kuwaelimisha wateja wao na kupunguza changamoto zinazoweza kujitokeza wakati wa kusafirisha bidhaa kupitia uwanja wa ndege.

“Kwa elimu tuliyopewa tutaweza kuwaelimisha wateja wetu na kuwasaidia kufanikiwa kupita na mizigo yao salama bila mizigo yao kubaki pale uwanja wa ndege,” amesema Mashugu.

Amesema elimu hiyo imewapa uelewa mpana kuhusu taratibu za kisheria na namna ya kufanya biashara ya mazao ya misitu kwa usahihi.

TFS imeendelea kusisitiza umuhimu wa wafanyabiashara na wadau wa mazao ya misitu kufuata sheria, kanuni na taratibu zilizowekwa, huku ikiwataka kupata elimu na vibali kutoka katika ofisi husika za Serikali kabla ya kuanza biashara au kusafirisha bidhaa hizo nje ya nchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!