Na Adery Masta .
Shirika la Viwango Tanzania (TBS) Kanda ya Magharibi linaendelea kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi na wajasiriamali katika Maonesho ya Wakulima ya Nane Nane yanayoendelea katika Viwanja vya Fatuma Mwasa (Ipuli), mkoani Tabora, ikiwa ni sehemu ya juhudi za Serikali kuhakikisha bidhaa zinazozalishwa nchini zinakidhi viwango vinavyotakiwa na kupata ushindani katika soko la ndani na nje ya nchi.


Katika maonesho hayo, TBS inatoa huduma za usajili wa bidhaa, udhibiti wa ubora, ushauri wa kitaalamu pamoja na elimu kuhusu umuhimu wa kuzingatia viwango katika uzalishaji wa bidhaa. Huduma hizo zimeendelea kuwavutia wajasiriamali, wazalishaji na wafanyabiashara wanaotembelea banda la TBS kwa lengo la kupata maarifa yatakayowawezesha kukuza biashara zao.
Akizungumza katika maonesho hayo, Meneja wa TBS Kanda ya Magharibi, Bw. Hamisi Seleleko, amesema kuwa upatikanaji wa Alama ya Ubora ya TBS ni mchakato ulio rahisi kwa mzalishaji anayezingatia matakwa ya viwango, akiwataka wajasiriamali kuitumia fursa hiyo ili kuongeza thamani ya bidhaa zao na kujenga imani kwa walaji.

Amesema TBS imeendelea kutoa elimu na mwongozo kwa wazalishaji ili kuhakikisha bidhaa zao zinakidhi viwango vinavyotakiwa, hatua ambayo imekuwa chachu ya kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko mbalimbali.
Ushuhuda wa mafanikio hayo umeonekana kutoka kwa wazalishaji wa Tanzania Honey, ambao hivi karibuni walipatiwa Alama ya Ubora ya TBS. Wamesema hatua hiyo imeleta mabadiliko makubwa katika biashara yao kwa kuongeza imani ya wanunuzi na kufungua fursa mpya za masoko ya kimataifa.

Mmoja wa wazalishaji wa asali hiyo amesema tangu walipopata Alama ya Ubora ya TBS, bidhaa yao imeanza kuvuka mipaka ya Tanzania na kupata wateja kutoka mataifa mbalimbali, jambo ambalo limeongeza thamani ya biashara yao na kuwapa matumaini makubwa ya kupanua uzalishaji.
Aidha, mmoja wa wanawake wanaojihusisha na uzalishaji wa asali hiyo amesema tayari wamepokea mawasiliano kutoka kwa mwekezaji wa nchini India ambaye ameonesha nia ya kufanya biashara nao baada ya kujiridhisha kuwa bidhaa yao imeidhinishwa kwa Alama ya Ubora ya TBS.

“Wanunuzi wa kimataifa wanaangalia zaidi ubora na uaminifu wa bidhaa. Kupata Alama ya Ubora ya TBS kumetufungulia milango ambayo hapo awali ilikuwa vigumu kuifikia. Leo tunazungumza na wanunuzi kutoka nje ya nchi kwa kujiamini,” amesema.
Wazalishaji hao wameishukuru TBS pamoja na Serikali kwa kuendelea kuwawezesha wajasiriamali kupitia utoaji wa elimu, ushauri wa kitaalamu na huduma za uthibitishaji wa ubora ambazo zimekuwa msingi wa kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini.
Ushiriki wa TBS katika Maonesho ya Nane Nane unaendelea kuthibitisha dhamira ya taasisi hiyo ya kuhakikisha bidhaa za Tanzania zinakidhi viwango vya ubora, zinawalinda walaji na kuwapa wazalishaji uwezo wa kushindana katika masoko ya kikanda na kimataifa.
Kupitia kaulimbiu ya kuongeza thamani ya mazao na bidhaa za Tanzania, TBS inaendelea kuwahimiza wajasiriamali wote kutumia huduma zake ili kupata Alama ya Ubora, hatua inayochochea ukuaji wa biashara, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi wa Taifa.









