Home Kitaifa TBA YANG’ARA SABASABA, YASHINDA TUZO YA BANDA BORA KATIKA SEKTA YA MILIKI...

TBA YANG’ARA SABASABA, YASHINDA TUZO YA BANDA BORA KATIKA SEKTA YA MILIKI NA REAL ESTATE

Na Magrethy Katengu–Dar es salaam

Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umeibuka mshindi wa nafasi ya pili na kutunukiwa tuzo ya Banda Bora katika Sekta ya Miliki na Real Estate wakati wa sherehe za kufunga Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba yaliyofanyika jijini Dar es Salaam.

Tuzo hiyo ilipokelewa kwa niaba ya Mtendaji Mkuu wa TBA, Arch. Daud W. Kondoro, na Mkurugenzi wa Huduma Saidizi wa TBA, Bi. Amina Lumuli, ambaye amesema mafanikio hayo yametokana na ubunifu mkubwa uliotumika katika maandalizi ya banda la taasisi hiyo pamoja na namna lilivyowasilisha kwa ufanisi fursa mbalimbali za uwekezaji kwa wananchi na wadau wa maendeleo.

Akizungumza na waandishi wa habari,Julai 13, 2026 Bi. Lumuli amesema TBA imeweka mkazo katika kuhamasisha uwekezaji kupitia mfumo wa Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP), huku ikitoa elimu kuhusu miradi ya kimkakati inayotekelezwa na wakala huo katika maeneo mbalimbali nchini.

Ameeleza kuwa baadhi ya miradi iliyovutia idadi kubwa ya wageni waliotembelea banda la TBA ni ujenzi wa nyumba za gharama nafuu, majengo ya serikali pamoja na ukarabati na uboreshaji wa miundombinu ya michezo, ikiwemo Uwanja wa Benjamin Mkapa. Amesema miradi hiyo inaonesha uwezo wa kitaalamu wa TBA katika sekta ya ujenzi na usimamizi wa majengo.

Bi. Lumuli amesema tuzo hiyo ni uthibitisho wa imani ambayo wananchi na wadau wanaendelea kuiweka kwa TBA kutokana na utoaji wa huduma bora, ubunifu wa kihandisi na utekelezaji wa miradi yenye tija kwa maendeleo ya Taifa. Aidha, ametoa wito kwa wawekezaji kujitokeza na kutumia fursa zilizopo kupitia miradi ya ubia inayotekelezwa na wakala huo.

Sherehe za utoaji wa tuzo na kufungwa kwa Maonesho ya 50 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba ziliongozwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi, ambapo TBA iliendelea kutajwa miongoni mwa taasisi za serikali zinazofanya vizuri katika utoaji wa huduma, ubunifu wa kihandisi na kuvutia wawekezaji nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!