Home Kitaifa WAZIRI MKUU MGENI RASMI UZINDUZI WA KITABU CHA “MAMA SAMIA DOCTRINE OF...

WAZIRI MKUU MGENI RASMI UZINDUZI WA KITABU CHA “MAMA SAMIA DOCTRINE OF LAW”

Na Magrethy Katengu-Dar es Salaam

Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania, TPBA, kimetangaza rasmi uzinduzi wa kitabu kipya cha “Falsafa ya Sheria ya Mama Samia” – Mama Samia Doctrine of Law, sambamba na maandalizi ya Mkutano wake Mkuu wa Mwaka 2026.

Akizungumza na waandishi wa habari, Makamu wa Rais wa chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania TPBA, Debora Mcharo, amesema kitabu hicho kinatoa mwangaza kuhusu mwelekeo na mafanikio ya utawala wa Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

“Kitabu hiki ni muhimu sana kwa kila Mtanzania. Kinatueleza historia, falsafa na mafanikio ya nchi yetu chini ya uongozi wa Rais Samia. Tunawaomba wananchi wote wajitokeze kukisoma ili kuelewa vizuri mwelekeo wa nchi,” alisema Bi. Mcharo.

Bi. Mcharo amebainisha kuwa uzinduzi wa kitabu hicho unatarajiwa kufanyika tarehe 10 Julai 2026, saa 2:00 asubuhi, katika Maktaba Mpya ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, (UDSM) na Mgeni Rasmi katika uzinduzi huo anatarajiwa kuwa *Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Mwigulu Lameck Nchemba.

Aidha, TPBA inatarajia kufanya Mkutano wake Mkuu wa Mwaka 2026 kuanzia tarehe 13 hadi 14 Julai 2026, katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano wa AICC, Jijini Arusha,na katika Mkutano huo, Mgeni Rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.

Kwa mujibu wa Bi. Mcharo, mkutano huo utaiunganisha familia nzima ya Mawakili wa Serikali kutoka Tanzania nzima ili kutathmini utekelezaji wa majukumu kwa mwaka uliopita na kupanga mikakati thabiti kwa mwaka ujao.

“Mkutano huu ni jukwaa letu la kujipima, kubadilishana uzoefu na kuweka mipango itakayoiwezesha TPBA kuendelea kutoa huduma bora za kisheria kwa Serikali na wananchi,” alifafanua.

Kwa upande wake, Katibu wa chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania (TPBA) Rashid Mohamed Said, amesema uzinduzi wa kitabu hicho una umuhimu mkubwa kwa umma kwani unaeleza kwa kina falsafa ya utawala na sheria katika kipindi hiki.

“Nawaomba wananchi watenge muda na waje kusikiliza moja kwa moja yaliyomo katika kitabu hiki. Ni somo kubwa kwa taifa letu,” alisema Rashid.

Naye Mweka Hazina wa TPBA,Andrew Kevela, amesema uzinduzi huo ni fursa ya kipekee kwa wananchi kukutana na viongozi mbalimbali wa Serikali.

“Tunatarajia Mawaziri zaidi ya kumi kushiriki katika uzinduzi huu. Ni fursa kwa wananchi kuonana na viongozi wao na kupata uelewa mpana wa sera na sheria za nchi,” alisema.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!