Home Kitaifa MIRADI 73 KUZINDULIWA NA MWENGE MKOANI TANGA

MIRADI 73 KUZINDULIWA NA MWENGE MKOANI TANGA

Na Zabela Mponji, TANGA

Miradi 73 yenye thamani ya Bil. 27.3 katika Halmashauri zote 11 za Mkoa wa Tanga inatarajiwa kuzinduliwa na Mbio za Mwenge, ambao unatarajiwa kuwasili mkoani Tanga Juni 17 ukitokea mkoani Morogoro.

Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk. Batilda Burian, amewaambia waandishi wa habari ofisini kwake kuwa Mwenge huo unatarajia kuwasili mkoani hapa Tanga katika viwanja vya Mji Mpya wilayani Kilindi, ambapo utazunguka Halmashauri zote 11 hadi Juni 28 utakapokabidhiwa mkoani Kilimanjaro.

Dk. Batilda amesema maandalizi ya ujio wa Mwenge huo yamekamilika na amewaomba wananchi kujitokeza kwa wingi kuupokea Mwenge.

“Maandalizi ya ujio wa Mwenge yamekamilika. Nawaomba wananchi na wadau wa maendeleo wa Mkoa wa Tanga mjitokeze kwa wingi ili kuupokea Mwenge pamoja na kuzindua miradi mbalimbali ya maendeleo katika mkoa wetu. Tunatarajia kuwa na miradi kwenye kila Halmashauri, hivyo wananchi ni vyema mkajitokeza kwa wingi kuunga mkono jitihada za Serikali katika utekelezaji wa miradi ya wananchi,” alisisitiza Dk. Batilda.

Kwa upande wao, baadhi ya wananchi wa Mkoa wa Tanga wameonyesha kufurahishwa na ujio wa Mwenge, ikizingatiwa kuwa Mkoa wa Tanga una miradi mikubwa ya kimkakati kama vile bomba la mafuta na bandari.

“Mimi kama mkazi wa Tanga nina shauku kubwa ya kuupokea Mwenge kwani mkoa wetu una miradi mikubwa. Kama tunavyoona, bandarini kwetu muda wote kazi zinafanyika na magari yanaingia na kutoka, hususan magari makubwa. Hivyo mimi kama bodaboda nafurahia sana ujio wa Mwenge kwa sababu kwangu ni fursa kubwa ya kuongeza kipato,” alisema Bakari Juma.

Kwa upande wake, Mwanaidi Hamisi alisema ujio wa Mwenge ni fursa kubwa kwani mahali utakapofikia Mwenge ndipo kituo chake cha biashara ya mama lishe kilipo.

“Nina furaha kubwa kwa ujio huu wa Mwenge katika mkoa wetu kwani utatusaidia kupata mapato makubwa, hasa sisi mama lishe wa eneo hili ambapo tutaupokea Mwenge,” alisema Mwanaidi, mfanyabiashara wa vyakula.

MWISHO

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!