Home Kitaifa DKT. SHEKALAGHE AWATAKA WADAU KUENDELEA KUUNGA MKONO MAPAMBANO DHIDI YA VIFO VYA...

DKT. SHEKALAGHE AWATAKA WADAU KUENDELEA KUUNGA MKONO MAPAMBANO DHIDI YA VIFO VYA MAMA NA MTOTO

Na Abdu Madenge, WAF – Dar es Salaam

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dkt. Seif Shekalaghe, ametoa wito kwa wadau wa maendeleo kuendelea kuunga mkono juhudi za Serikali katika kuboresha afya ya uzazi kwa kutoa msaada wa kifedha, kiufundi na rasilimali nyingine muhimu, huku akisisitiza dhamira ya Serikali ya kutokomeza au kupunguza kwa kiwango kikubwa vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika.

Dkt. Shekalaghe amesema hayo tarehe 13 Juni, 2026 jijini Dar es Salaam wakati akifunga Kikao cha Kamati ya Kitaalam (TWG 5) ya Masuala ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto.

Akizungumzia umuhimu wa ushiriki wa wadau wa maendeleo, Mkurugenzi wa Idara ya Afya ya Uzazi, Mama na Mtoto kutoka Wizara ya Afya, Dkt. Ahmad Mohammed Makuwani, amesema kikao hicho hufanyika kila robo mwaka kwa lengo la kuwaleta pamoja wataalamu na wadau wa maendeleo ili kupitia utekelezaji wa afua za afya ya uzazi, mama na mtoto na kujadili maeneo ya kipaumbele yatakayosaidia kufikia malengo ya mwaka wa fedha 2024/2025.

Amesema mijadala ya kikao hicho inaongozwa na malengo yaliyoainishwa katika Mpango Mkakati wa RMNCAH One Plan III (2021/22–2025/26), huku ushirikiano wa Serikali na wadau ukiendelea kuwa nguzo muhimu katika kuharakisha utekelezaji wa afua zinazolenga kupunguza vifo vya akina mama wajawazito na watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika.

“Ombi langu ni kwamba wadau wote waendelee kutuunga mkono kifedha, kiufundi na kwa namna nyingine mbalimbali. Sisi kama viongozi jukumu letu ni kusikiliza ushauri wa wataalamu na kuugeuza kuwa sera na mipango inayoweza kutekelezwa kwa manufaa ya wananchi,” alisema Dkt. Shekalaghe.

Aliongeza kuwa Wizara ya Afya itaendelea kutoa nafasi kwa wataalamu kutoa mapendekezo na ushauri utakaosaidia kuimarisha afua za afya ya uzazi, mama na mtoto ili kuhakikisha huduma bora zinaendelea kuwafikia wananchi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!