Home Kitaifa MBUNGE SHABIBY AIPONGEZA WMA KWA KULINDA MASLAHI YA WANANCHI NA KUSIMAMIA VIPIMO...

MBUNGE SHABIBY AIPONGEZA WMA KWA KULINDA MASLAHI YA WANANCHI NA KUSIMAMIA VIPIMO SAHIHI

Mbunge wa Jimbo la Gairo, Ahmed Shabiby, ameupongeza Wakala wa Vipimo Tanzania (WMA) kwa kazi kubwa inayofanya katika kuhakikisha wananchi wanapata huduma na bidhaa zenye vipimo sahihi, hatua ambayo amesema imeendelea kuimarisha ulinzi wa maslahi ya walaji pamoja na wafanyabiashara nchini.

Akichangia leo Mei 22,bungeni Dodoma wakati wa mjadala wa Makadirio ya Mapato na Matumizi ya Wizara ya Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Shabiby amesema  WMA imeendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi mkubwa huku ikishirikiana kikamilifu na wadau mbalimbali kuhakikisha mfumo wa usimamizi wa vipimo nchini unakuwa imara na wa kuaminika.

Shabiby amesema  WMA imekuwa mstari wa mbele kutoa ushirikiano wa karibu kila inapohitajika, jambo lililochangia kuongezeka kwa ufanisi katika usimamizi wa vipimo nchini na kuimarisha imani ya wananchi kwa taasisi hiyo..

Aidha, amempongeza Afisa Mtendaji Mkuu wa WMA, Alban Kihulla, kwa uongozi wake wenye weledi, uwajibikaji na ushirikiano mzuri katika kusimamia majukumu ya wakala huo muhimu kwa maendeleo ya sekta ya biashara na viwanda.

Hata hivyo, mbunge huyo ameitaka WMA kuongeza umakini zaidi katika kudhibiti ubora wa bidhaa za chuma, hususan nondo zinazozalishwa na baadhi ya viwanda nchini, akieleza kuwa bado kuna changamoto ya uwepo wa bidhaa zisizokidhi viwango vya vipimo vinavyotakiwa.

Amesema baadhi ya viwanda vinavyoendeshwa na wawekezaji wa ndani na nje ya nchi vinaendelea kuzalisha nondo zenye upungufu wa vipimo, hali inayoweza kuhatarisha usalama wa majengo pamoja na maisha ya wananchi.

“Tusibaki kwenye kutoa faini pekee. Viwanda vinavyotengeneza nondo zisizokidhi vipimo vinapaswa kuchukuliwa hatua kali ikiwemo kufungiwa, ili kulinda usalama wa wananchi na kuhakikisha ubora wa ujenzi nchini,” amesema  Shabiby.

Ameongeza kuwa usimamizi madhubuti wa vipimo vya bidhaa za ujenzi ni msingi muhimu katika kukuza sekta ya viwanda, kulinda miundombinu na kuhakikisha maendeleo endelevu ya taifa.

 Wakala wa Vipimo Tanzania umeendelea kusimamia matumizi sahihi ya vipimo nchini kwa mujibu wa Sheria ya Vipimo Sura ya 340, ikiwa ni jitihada za kuhakikisha wananchi wanapata bidhaa sahihi kulingana na thamani ya fedha wanazolipa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!