Home Biashara MAUZO YA BIDHAA NJE YAFIKIA DOLA BILIONI 10

MAUZO YA BIDHAA NJE YAFIKIA DOLA BILIONI 10

WAZIRI wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema biashara ya Tanzania na mataifa ya nje imeendelea kuimarika huku thamani ya mauzo ya bidhaa nje ya nchi ikiongezeka kwa asilimia 16 mwaka 2025.

Akiwasilisha bungeni makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara kwa mwaka wa fedha 2026/2027, Kapinga amesema mauzo ya bidhaa nje ya nchi yaliongezeka kutoka dola za Marekani milioni 8,702 mwaka 2024 hadi dola milioni 10,080.9 mwaka 2025.

Amesema mafanikio hayo yametokana na kuendelea kuboreshwa kwa mazingira ya biashara nchini, upanuzi wa masoko ya bidhaa za Tanzania pamoja na utekelezaji wa mikakati ya kuongeza ushindani wa bidhaa katika soko la kimataifa.

Kapinga ameeleza kuwa Serikali imeendelea kupunguza urasimu katika usafirishaji wa bidhaa nje ya nchi sambamba na kuhamasisha uzalishaji wa bidhaa zinazokidhi viwango vya kimataifa.

Baadhi ya bidhaa zilizouzwa kwa wingi nje ya nchi ni mazao ya kilimo yakiwemo ufuta, tumbaku, mbaazi, ngano, mchele, maharage, mahindi, kahawa, pamba na parachichi.

Ametaja bidhaa nyingine kuwa ni mazao ya mifugo na uvuvi, ikiwemo samaki, pamoja na bidhaa za viwandani kama dhahabu, kakao, makaa ya mawe, vigae na mabati.

Kwa upande wa bidhaa zinazoingizwa nchini, Kapinga amesema mwaka 2025 Tanzania iliagiza bidhaa zenye thamani ya dola za Marekani milioni 16,031.3 ikilinganishwa na dola milioni 15,684.5 mwaka 2024, sawa na ongezeko la asilimia 2.2.

Amefafanua kuwa ongezeko hilo limetokana na kuagizwa kwa bidhaa ambazo bado hazizalishwi nchini pamoja na bidhaa zinazohitaji teknolojia ya juu.

Bidhaa zilizoagizwa kwa wingi ni pamoja na bidhaa za mitaji, magari, vifaa vya kutengeneza lami, bidhaa za chuma, mashine za hospitali, dawa za baridi, mafuta ya petroli na gesi pamoja na sukari ya viwandani.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!