
Daudi Nyingo – DODOMA
Bodi ya Ushauri ya Wakala ya Maabara ya Veterinari Tanzania (TVLA) imeeleza kuridhishwa kwake na maendeleo ya mradi mkubwa wa ujenzi wa jengo la ofisi na maabara ya kisasa unaotekelezwa katika Kituo cha Kanda ya Kati jijini Dodoma ambapo Mradi huo wenye ghorofa nne unategemewa kuwa mradi kielelezo nchini utakapokamilika.
Akizungumza wakati wa ziara ya ukaguzi katika eneo la ujenzi Mei 15, 2026, Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri ya TVLA, Prof. Amandus P. Muhairwa, alipongeza kasi ya mkandarasi na ubora wa kazi inayofanyika kwa kuwa awamu ya kwanza ya mradi huo ulioanza mwezi Oktoba 2025 na unatarajiwa kukamilika Oktoba 2026, tayari umefikia takriban asilimia 60% ya ujenzi.
“Kwa nilivyoangalia hali ya majengo waliyoyajenga na vifaa vilivyotumika, ubora wake ni wa juu, hilo naweza kuwapongeza sana wajenzi pamoja na wasimamizi wa ujenzi na mamlaka ya TVLA kwa kusimamia na kutoa mahitaji yanayotakiwa kwa wakati,” alisema Prof. Muhairwa.
Aidha, alibainisha kuwa vifaa vinavyotumika kama nondo na zege ni vya hali ya juu, jambo linaloonyesha thamani halisi ya fedha (Value for Money) zinazowekezwa na alipongeza hali ya usalama wa wafanyakazi saiti, akisema kuwa wote wana vitendea kazi na vifaa vya kujikinga (PPE).
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa TVLA, Dkt. Stella Bitanyi, alieleza kuwa mradi huo unagharimu takriban Shilingi Bilioni 6 na unatekelezwa kwa kutumia fedha za makusanyo ya ndani ya wakala. Alibainisha kuwa ujenzi huo unatekelezwa na Mkandarasi ambaye ni Kikosi cha Ujenzi na umefikia hatua ya nguzo baada ya msingi kukamilika.
“Tunashukuru serikali kwa kutuwezesha kibajeti na kupata fedha za mapato ya ndani zinazotumika kwenye mradi huu. Tutakuwa na maabara ya kisasa kabisa itakayohudumia wafugaji wa Kanda ya Kati na mikoa jirani,” alisema Dkt. Bitanyi.
Dkt. Bitanyi aliongeza kuwa uamuzi wa kujenga maabara hiyo Dodoma ni wa kimkakati kufuatia shughuli nyingi za serikali kuhamia jijini humo. Lengo ni kuwa na maabara yenye hadhi ya makao makuu yenye uwezo wa kutoa huduma bora kwa jamii, taasisi za umma, na wafugaji binafsi.
Uongozi wa TVLA uliishukuru Wizara ya Mifugo na Uvuvi kupitia kwa Waziri na Katibu Mkuu kwa ushirikiano mkubwa unaohakikisha mradi unakamilika kwa wakati uliopangwa.









