Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Mhe. Balozi Meja Jenerali (Mstaafu), Jacob Kingu amelipongeza Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) kwa utekelezaji wa mradi wa nishati safi ya kupikia katika kambi zake, huku akiwahamasisha kuelimisha jamii zinazozunguka kambi hizo nazo kutumia nishatia nishati safi ya kupikia.
Pongezi hizo zimetolewa leo Mei 9, 2026 wakati wa ziara ya Bodi hiyo iliyolenga kukagua utekelezaji wa miradi ya nishati safi ya kupikia inaayotekelezwa na Wakala wa Nishati Vijijini (REA) katika Kambi ya JKT ya Oljoro Jijini Arusha.
Mradi huo unahusisha uzalishaji wa bayogesi kupitia mbolea ya ng’ombe, matumizi ya majiko ya gesi, majiko banifu na mashine za kutengenezea mkaa mbadala.
Mwenyekiti Kingu pia, amesisitiza juu ya vijana waliopo kwenye kambi hizo za JKT kupatiwa mafunzo ya namna ya kutengeneza mkaa mbadala ili waweze kutumia ujuzi huo kujiajiri na kuwa mawakala wa kutengeneza mkaa mbadala pindi watakapomaliza mafunzo yao.
Kwa upande wake, akimwakilisha Mkuu wa JKT, Kanali Projest Rutaihwa aliishukuru Bodi hiyo pamoja na Menejimenti ya REA kwa utekelezaji wa miradi nishati safi ya kupikia ambapo kambi 22 zimepata fedha kutoka REA za utekelezaji wa mradi huo ili kulinda mazingira pamoja na afya za wanaoandaa chakula.
Naye Kamanda wa Kikosi cha 833 KJ Oljoro, Kanali Victor Rutayuga Faustine, amesema mradi huo wa nishati safi ya kupikia umeleta mafanikio makubwa katika utunzaji wa mazingira na kupunguza matumizi ya kuni kambini hapo pamoja na kutumia muda mdogo kwenye kuandaa chakula cha vijana wanaopata mafunzo kambini hapo.
“Kabla ya mradi huu tulikuwa tunaagiza lori la kuni kutoka Mbeya kwa ajili ya kupikia chakula cha vijana wetu wa mafunzo hapa kambini. Lakini sasa matumizi ya nishati safi yamesaidia kupunguza utegemezi huo na kulinda mazingira,” amesema Kanali Faustine.
REA imetoa ruzuku ya zaidi ya shilingi bilioni 5.2 kwa ajili ya kuwezesha matumizi ya nishati safi ya kupikia katika kambi za JKT ambapo fedha hizo pamoja na mambo mengine, zimewezesha kufungwa kwa mifumo ya nishati safi ya kupikia pamoja na ununuzi wa mashine za kutengenezea mkaa mbadala.



























