Home Kitaifa SERIKALI KUIMARISHA USHIRIKIANO NA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI

SERIKALI KUIMARISHA USHIRIKIANO NA MASHIRIKA YASIYO YA KISERIKALI

Na Saidina Msangi, WF, Dodoma

Wizara ya Fedha imebainisha kuwa itaendelea kujenga uelewa, kubadilishana uzoefu na kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na mashirika yasiyo ya kiserikali nchini ili kuhakikisha utekelezaji wa miradi ya maendeleo ya kijamii unakuwa na ufanisi mkubwa.

Hayo yalibainishwa na Kaimu Kamishna Msaidizi, Idara ya Fedha za Nje, Wizara ya Fedha, Bw. John Kuchaka, wakati akifungua warsha iliyowakutanisha Serikali na wadau wa mashirika yasiyo ya kiserikali, iliyofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Mkandarasi, jijini Dodoma.

Alisema jitihada za Serikali ya Tanzania zimekuwa zikilenga kuhakikisha kuwa maendeleo ya wananchi yanapatikana kwa njia jumuishi na endelevu, ambapo mchango wa mashirika hayo ni muhimu katika kufikisha huduma kwa jamii na kuunga mkono juhudi za Serikali katika sekta mbalimbali.

Kupitia warsha hii, mafunzo yatatolewa kuhusu masuala muhimu, ikiwemo mwongozo wa kufuata taratibu za kifedha kwa wadau wasio wa kiserikali, mwongozo wa bajeti ya Serikali pamoja na miongozo ya uratibu na ushirikiano wa maendeleo ili kuwa na uelewa wa pamoja kuhusu mifumo na taratibu zinazosimamia shughuli hizo,” alifafanua Bw. Kuchaka.

Aliongeza kuwa kupitia mafunzo hayo, Serikali inatarajia kujenga uwezo wa wadau wote katika kuhakikisha kuwa shughuli za mashirika zinaendana na vipaumbele vya taifa huku zikifuata taratibu zilizowekwa kwa ajili ya kuleta matokeo chanya kwa wananchi.

Bw. Kuchaka alitoa rai kwa washiriki hao kutumia fursa hiyo kubadilishana uzoefu na kubaini maeneo ya kuboresha ushirikiano huku msisitizo ukiwekwa katika kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utekelezaji wa miradi yote ya maendeleo nchini.

Nao baadhi ya washiriki wa warsha hiyo, akiwemo Mkurugenzi wa Shirika la Doyodo Tanzania, Rajabu Juma, pamoja na Msajili Msaidizi wa Mashirika Yasiyo ya Kiserikali mkoani Manyara, Bi. Anna Emmanuel, wamesema mafunzo hayo yatawasaidia kuimarisha mazingira ya ushirikiano na kuongeza ufanisi katika utekelezaji wa majukumu yao ili jamii iendelee kunufaika na huduma zinazotolewa na mashirika yasiyo ya kiserikali.

Warsha hiyo ya siku moja iliwakutanisha wadau kutoka Serikalini na mashirika yasiyo ya kiserikali kutoka mikoa ya Kigoma, Dodoma, Kagera, Mara, Manyara, Tabora, Rukwa, Singida, Shinyanga, Simiyu, Geita na Arusha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!