Home Kitaifa IDARA YA KUMBUKUMBU NA NYARAKA ZA TAIFA KUIMARISHA UHIFADHI WA HISTORIA YA...

IDARA YA KUMBUKUMBU NA NYARAKA ZA TAIFA KUIMARISHA UHIFADHI WA HISTORIA YA TAIFA 2026/27

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027 leo Aprili 17,2026 bungeni Dodoma.

Na.Alex Sonna-DODOMA

Serikali kupitia Ofisi ya Rais, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa imepanga kutekeleza mageuzi makubwa katika uhifadhi na usimamizi wa taarifa za taifa kwa mwaka wa fedha 2026/27, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha utunzaji wa historia na kuongeza ufanisi katika utoaji wa huduma za umma.

Hayo yamesemwa leo Aprili 17,2026 bungeni Dodoma na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais,Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Ridhiwani Kikwete, akiwasilisha Hotuba ya Bajeti kwa Mwaka wa Fedha 2026/2027.

Amesema kuwa idara imejipanga kukusanya taarifa, kumbukumbu, nyaraka na machapisho mbalimbali yanayohusu historia ya nchi kutoka taasisi za umma na watu binafsi, hatua itakayosaidia kulinda na kuhifadhi urithi wa taifa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

Aidha, juhudi maalum zitafanyika kutambua, kukusanya na kuhifadhi kumbukumbu na vitu vya waasisi wa taifa pamoja na Marais wote wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama sehemu ya kulinda historia ya uongozi wa nchi.

Katika kuimarisha mifumo ya utendaji serikalini, idara itaweka na kuhuisha mifumo ya kisasa ya utunzaji wa kumbukumbu ikiwemo Keyword Filing System na e-File Management System katika taasisi mbalimbali za umma, ili kuongeza ufanisi na kasi ya utoaji huduma.

Vilevile, idara itaimarisha matumizi ya teknolojia ya kidijitali kupitia mfumo wa Digital Records Management and Preservation System, ambao utasaidia kuhifadhi nyaraka kwa njia ya kisasa, kurahisisha upatikanaji wake na kulinda nakala halisi dhidi ya uharibifu.

Katika kuboresha usimamizi wa taarifa, taasisi za umma zitasaidiwa kuandaa miongozo ya uhifadhi na uteketezaji wa kumbukumbu, pamoja na kufanya tathmini ya kumbukumbu tuli ili kuhakikisha zinatunzwa kwa viwango vinavyotakiwa.

Aidha, idara itajenga uwezo wa watumishi wa umma kupitia mafunzo, mikutano ya kitaalamu na warsha zinazolenga kuongeza uelewa kuhusu sheria, kanuni na taratibu za utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka za Serikali.

Pia, wananchi wataelimishwa kuhusu umuhimu wa utunzaji wa kumbukumbu kama nyenzo muhimu ya maendeleo ya taifa, sambamba na kuimarishwa kwa ukaguzi na uhamishaji wa kumbukumbu tuli kutoka taasisi mbalimbali kwenda vituo vya hifadhi ya taifa.

Kwa ujumla, mpango huu unaonesha dhamira ya Serikali ya kulinda historia ya taifa, kuimarisha uwazi na kuongeza ufanisi katika usimamizi wa taarifa kupitia matumizi ya mifumo ya kisasa ya kidijitali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!