Home Kitaifa TAARIFA MUHIMU KUTOKA PDPC KWA TAASISI ZINAZOKUSANYA NA KUCHAKATA TAARIFA BINAFSI.

TAARIFA MUHIMU KUTOKA PDPC KWA TAASISI ZINAZOKUSANYA NA KUCHAKATA TAARIFA BINAFSI.

 Na Mwandishi Wetu.

Zimesalia siku chache kabla ya kufikiwa kwa ukomo wa usajili wa hiari kwa taasisi zinazokusanya na kuchakata taarifa binafsi nchini. Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) imetangaza kuwa ifikapo tarehe 9 Aprili mwaka huu, itaanza kuchukua hatua kali za kisheria ikiwemo faini ya hadi shilingi bilioni tano kwa taasisi zitakazokiuka taratibu hizo.

Tume ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi (PDPC) leo Machi 26, 2026 imetoa msisitizo wa mwisho kwa taasisi zote za umma na binafsi nchini, ikizikumbusha kuwa muda wa usajili wa hiari unafikia tamati tarehe 8 Aprili, 2026.

Akizungumza kwenye mkutano na waandishi wa habari, Mkurugenzi Mkuu wa Tume hiyo, Dkt. Emmanuel Lameck Mkilia, amesema kuwa serikali imetoa muda wa kutosha tangu mwaka 2024 ili kutoa fursa kwa taasisi kujipanga.

“Serikali ilitoa muda wa kutosha wa kujisajili. Muda huo ulianza Aprili 2024 wakati Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alipozindua Tume. Muda uliongezwa mara mbili, mara ya mwisho ikiwa ni uamuzi wa Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Mhe. Angellah Jasmine Mbelwa Kairuki, ambaye aliweka tarehe ya mwisho kuwa tarehe 8, Aprili, mwaka huu” amesema Dkt. Mkilia

Dkt. Mkilia amebainisha kuwa, kuanzia tarehe 9 Aprili, 2026, utekelezaji wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi Sura ya 44 utaanza rasmi, na taasisi yoyote itakayobainika kutokujisajili kwenye mfumo wa PDPC itawajibika kisheria.

“Kwa mujibu wa Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi, adhabu kwa mtu binafsi ni faini ya kuanzia Shilingi za kitanzania laki moja hadi Milioni 20 au kifungo cha hadi miaka 10 jela. Kwa upande wa taasisi na makampuni, adhabu ni faini kuanzia Shilingi Milioni moja hadi kufikia kiasi cha Shilingi Bilioni Tano za kitanzania, kulingana na aina ya ukiukwaji.

Sheria ya Ulinzi wa Taarifa Binafsi inazigusa sekta zote muhimu zikiwemo Wizara na idara za Serikali, mabenki, kampuni za bima, hospitali, shule, vyuo, kampuni za simu, viwanda, sekta ya utalii, hoteli, kampuni za usafirishaji, kampuni za ujenzi, vyama vya siasa, vyama vya wafanyakazi, jumuiya za kidini, mashirika yasiyo ya kiserikali na taasisi nyingine nyingi.

Sheria hii ni ngao kwa mwananchi ambaye ndiye muhusika wa taarifa, kwani inalinda haki ya msingi ya faragha. Aidha, inajenga imani kati ya watoa huduma na wateja wao, jambo ambalo ni nguzo muhimu katika kukuza uchumi wa kidigitali na uwekezaji nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!