Home Kimataifa KAPINGA: USHIRIKIANO WA TANZANIA NA CHINA WAZAA MATOKEO MAKUBWA YA UWEKEZAJI NA...

KAPINGA: USHIRIKIANO WA TANZANIA NA CHINA WAZAA MATOKEO MAKUBWA YA UWEKEZAJI NA BIASHARA

Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, amesema kuwa mafanikio ya ushirikiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na China yanaendelea kuimarika kwa kasi katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan, yakionesha mwelekeo chanya wa ukuaji wa uwekezaji na biashara.

Akizungumza leo, Machi 22, 2026, katika ziara yake ya siku tatu nchini China iliyoandaliwa na Wizara ya Viwanda na Biashara kwa kushirikiana na Wizara ya Mipango na Uwekezaji, Kapinga amesema jumla ya miradi 876 ya uwekezaji kutoka China imetekelezwa nchini Tanzania, ikiwa na thamani ya dola za Kimarekani milioni 8,860.

Amesema miradi hiyo imezalisha ajira 146,250 kwa Watanzania, hatua inayochangia kwa kiasi kikubwa ukuaji wa uchumi wa taifa.

Kwa upande wa biashara, Kapinga amesema kiwango cha biashara kati ya Tanzania na China kimefikia dola bilioni 2, huku mauzo ya bidhaa za Tanzania kwenda China yakiongezeka kwa asilimia 12.5. Ameongeza kuwa takwimu hizo zinaonesha kuimarika kwa nafasi ya Tanzania katika soko la China.

Aidha, amebainisha kuwa mafanikio hayo yanachochewa na juhudi za kidiplomasia na kiuchumi zilizofanywa na Rais Samia, ikiwemo ziara yake nchini China mwaka 2022, iliyoweka msingi wa ushirikiano wa kimkakati unaoendelea kuzaa matunda.

Katika muktadha mpana wa maendeleo, amesema takwimu hizo zinaendana na malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050, inayolenga kufikisha uchumi wa Tanzania kufikia thamani ya takribani dola za Kimarekani trilioni 1. Ameongeza kuwa sekta binafsi inatarajiwa kuchangia zaidi ya asilimia 70 ya mtaji wa uwekezaji.

Katika ziara hiyo, jumla ya makampuni 150 yameshiriki katika mikutano ya uwekezaji, ambapo makampuni 100 yalikutana jana na makampuni 50 yamekutana leo kujadiliana kwa pamoja, yakiwa tayari yamekwisha kuwekeza nchini Tanzania.

Mwenendo huu wa takwimu unaashiria kuimarika kwa uhusiano wa kiuchumi kati ya Tanzania na China, na unaweka msingi imara wa kufikia malengo ya muda mrefu ya kukuza uchumi kupitia uwekezaji na biashara ya kimataifa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!