Home Kitaifa BALOZI WA IRELAND NA NM-AIST WAJADILI UTEKELEZAJI WA SAMIA SCHOLARSHIP DS/AI+

BALOZI WA IRELAND NA NM-AIST WAJADILI UTEKELEZAJI WA SAMIA SCHOLARSHIP DS/AI+

Balozi wa Ireland nchini Tanzania, Mhe. Nicola Brennan na uongozi wa Taasisi ya Afrika ya Sayansi na Teknolojia ya Nelson Mandela (NM-AIST) wamejadiliana namna ya kuimarisha utekelezaji wa mpango wa Samia Scholarship Extended DS/AI+ unaolenga kujenga wataalamu wa Akili Bandia (AI) na Sayansi ya Takwimu (Data Science) nchini.

Akizungumza wakati wa ziara hiyo iliyofanyika tarehe 9 Machi 2026 katika Taasisi hiyo jijini Arusha, Makamu Mkuu wa NM-AIST, Prof. Maulilio Kipanyula, amesema katika awamu ya kwanza ya mpango huo wanafunzi 34 wa Kitanzania wamepata nafasi ya kusoma katika vyuo vikuu vya Ireland.

Ameongeza kuwa Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH) pamoja na NM-AIST inapanga kuandaa *bootcamp* maalum kwa ajili ya kuwaandaa wanafunzi watakaofuata kunufaika na mpango huo.

Kwa upande wake, Balozi Brennan ameipongeza Serikali ya Tanzania chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa dhamira ya kuwekeza katika elimu ya juu katika fani za AI, Data Science na Sayansi shirikishi, akibainisha kuwa wanafunzi wa Kitanzania watapata elimu yenye viwango vya kimataifa katika vyuo vikuu vya Ireland.

Aidha, amesisitiza umuhimu wa kuongeza ushiriki wa wanawake katika masomo ya STEM na kuhimiza taasisi na wabunifu kuhakikisha matokeo ya tafiti yanafika sokoni ili kuchangia maendeleo ya uchumi, usalama wa chakula na ajira.

Katika ziara hiyo, Balozi Brennan pia alitembelea maabara, kituo cha kompyuta chenye uwezo mkubwa (HPC), Data Driven Institute (DDI) pamoja na vituo vya ubunifu vya NM-AIST ili kujionea mchango wa taasisi hiyo katika maendeleo ya sayansi na teknolojia nchini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!