
Mchungaji wa Usharika wa Kijitonyama, Dk. Eliano Kimaro, amesema serikali yoyote duniani haiwezi kuajiri wahitimu wote, hivyo ni muhimu kuwepo kwa miradi ya familia itakayowezesha kujiajiri na kuajiri wengine. Pia amewasihi wanafunzi wa Shule ya Sekondari Christon kuwa na nidhamu bora katika maisha kwa kuwa ndiyo msingi wa mafanikio yao ya baadaye.
Akizungumza Machi 7, 2026 mkoani Pwani wakati wa mahafali ya nane ya kidato cha nne ya mwaka 2025 katika shule hiyo, Dk. Kimaro amewapongeza wanafunzi 100 waliopata ufaulu wa division one. Amesisitiza kuwa nidhamu ndiyo msingi wa mafanikio kwa mwanafunzi kwani humfanya kuheshimu walimu, wazazi na wenzake pamoja na kutumia muda wake vizuri katika masomo.

Aidha, amewataka viongozi wa serikali, dini na jamii kuendelea kuhamasisha miradi ya kifamilia kama njia ya kupunguza tatizo la ajira kwa vijana. Ameeleza kuwa waajiriwa wanapaswa kujiandaa mapema kwa maisha ya baada ya kustaafu kwa kuanzisha miradi itakayowawezesha kuendeleza uchumi wao na wa familia.
Dk. Kimaro pia amewahimiza wazazi kusimamia maadili ya watoto wao, akieleza kuwa mabadiliko ya sayansi na teknolojia yamechangia kupungua kwa misingi ya maadili katika jamii. Amesisitiza kuwa familia na jamii zina jukumu la kuhakikisha vijana wanalelewa katika maadili mema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Shule ya Sekondari Christon, Enrique Msuya, amesema shule hiyo inatoa elimu ya vitendo kwa kuwafundisha wanafunzi masuala ya kilimo, ufugaji na uzalishaji wa chakula cha wanyama ili kuwajengea uwezo wa kujitegemea na kuwa wajasiriamali.
Naye Mkuu wa Shule hiyo, Augustin Minja, amesema mafanikio ya shule yanatokana na msisitizo wa nidhamu, juhudi za walimu na ushirikiano wa wanafunzi katika kujifunza. Ameongeza kuwa shule imejikita katika nguzo za Mungu kwanza, nidhamu, taaluma na ujasiriamali, huku ikiweka mkazo pia katika elimu ya vitendo ili kuwaandaa wanafunzi kujitegemea na kuchangia maendeleo ya jamii na taifa.








