Home Kitaifa ZIARA YA WAZIRI MKUU ARUSHA KUKAGUA MIRADI YA BILIONI 194.2

ZIARA YA WAZIRI MKUU ARUSHA KUKAGUA MIRADI YA BILIONI 194.2

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kuanza ziara ya kikazi mkoani Arusha kuanzia Februari 22 hadi 24, 2026, ambapo atatembelea na kukagua miradi sita yenye thamani ya shilingi bilioni 194.2 katika wilaya za Arumeru, Arusha na Longido, pamoja na kuzungumza na wananchi.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake leo Jumamosi, Februari 21, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mheshimiwa CPA Amos Gabriel Makalla, amesema kuwa kesho Jumapili Waziri Mkuu ataweka jiwe la msingi katika mradi wa ujenzi wa bweni la kisasa la Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Sayansi cha Nelson Mandela, atakagua upanuzi wa miundombinu ya Hospitali ya Oltrumet, pamoja na kuzungumza na wananchi katika eneo la Ngaramtoni.

Amesema kuwa Februari 23, Waziri Mkuu atakuwa wilayani Longido ambako atatembelea na kupokea taarifa ya mradi mkubwa wa maji katika Kata ya Sinya. Pia atazindua mradi wa upanuzi wa Shule ya Sekondari Sinya uliowezesha shule hiyo kuwa na kidato cha tano na sita. Baadaye atatembelea Kituo cha Utoaji Huduma cha Pamoja (One Stop Border Post) Namanga na kisha kuzungumza na wananchi katika viwanja vya Shule ya Msingi Namanga.

Aidha, Mkuu huyo wa Mkoa amewaalika wananchi wote kujitokeza kwa wingi kushiriki katika ziara hiyo muhimu. Amesema siku ya tatu ya ziara hiyo, Waziri Mkuu atatembelea Wilaya ya Arusha ambako anatarajiwa kukagua maendeleo ya ujenzi wa Kituo Kikuu cha Mabasi cha Jiji la Arusha kilichopo eneo la Bondeni City, kuweka jiwe la msingi katika ujenzi wa Soko la Kilombero, pamoja na kuzungumza na wananchi kupitia mkutano wa hadhara utakaofanyika katika eneo hilo la soko jijini Arusha.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!