Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga,akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 24,2026 katika Mji wa Kiserikali Mtumba jijini Dodoma kuhusu mafanikio makubwa ya siku 100 katika sekta ya Viwanda na Biashara baada ya uchaguzi Mkuu.
Â
Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga,akizungumza na waandishi wa habari leo Januari 24,2026 katika Mji wa Kiserikali Mtumba jijini Dodoma kuhusu mafanikio makubwa ya siku 100 katika sekta ya Viwanda na Biashara baada ya uchaguzi Mkuu.
Â
Msemaji Mkuu wa Serikali na Katibu Mkuu wa Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw.Gerson Msigwa,akizungumza na waandishi wa habari wakati Wizara ya Viwanda na Biashara ikiwasilisha mafanikio makubwa ya siku 100 katika sekta ya Viwanda na Biashara baada ya uchaguzi Mkuu.
Na.Alex Sonna-DODOMA
SERIKALI ya awamu ya sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kupitia sekta ya viwanda na biashara zimezalisha zaidi ya ajira 18,000 za moja kwa moja na zisizo za moja kwa moja kwa makundi mbalimbali ikiwamo vijana ndani ya siku 100 tangu Uchaguzi Mkuu Oktoba, 2025 huku zaidi ya ajira milioni 6.5 zikilengwa katika miaka sita ijayo.
Kwa mujibu wa Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga, amesema ajira hizo zimetokana na utekelezaji wa mikopo ya wajasiriamali, uanzishaji wa mitaa ya viwanda, uwekezaji mkubwa wa viwanda, uchakataji wa mazao, biashara ya korosho, pamoja na miradi ya uchumi wa kijani.
Amesema kupitia mikopo ya SIDO pekee, ajira 546 zimezalishwa, kati ya hizo ajira 436 zikiwa za vijana. Katika mitaa ya viwanda ya SIDO Kigoma, Morogoro, Mbeya na Singida, jumla ya ajira 4,619 zimepatikana, huku vijana wakinufaika kwa kiwango kikubwa.
Pia, amesema viwanda vidogo na vya kati vilivyowekwa na TEMDO katika sekta ya nishati mbadala, mafuta ya kula na uchakataji wa muhogo vimezalisha zaidi ya ajira 600 za moja kwa moja na zaidi ya ajira 1,300 zisizo za moja kwa moja, nyingi zikiwa za vijana na wanawake.
Katika uwekezaji mkubwa wa viwanda kupitia NDC, ikiwemo TAMCO na Kongani ya Kigamboni, zaidi ya ajira 5,000 za moja kwa moja tayari zimezalishwa, huku viwanda vinavyoendelea kujengwa vikitarajiwa kuongeza maelfu zaidi.
Pamoja na hayo, amesema Mfumo wa stakabadhi za ghala kwa zao la korosho umezalisha zaidi ya ajira 7,000 rasmi na zisizo rasmi katika maghala, usafirishaji na uchakataji, wakati tafiti za madini adimu na miradi ya uchumi wa kijani ikitoa zaidi ya ajira 300 katika maeneo ya utafiti na uzalishaji wa nishati safi.
Aidha, mafunzo ya ujasiriamali na uatamizi wa biashara yaliyotolewa na CBE, SIDO na TBS yamewaandaa zaidi ya vijana 1,500 kuingia sokoni kwa kujiajiri na kuajiri wengine.








