
Na Magrethy Katengu
MAMLAKA ya Mapato Tanzania (TRA) imesema zaidi ya makampuni 300 yataunganishwa na mfumo wa kisasa wa usimamizi wa kodi za ndani ujulikanao kama “Integrated Domestic Revenue Administration System (IDRAS)” ili kutatua kero mbalimbali za huduma za kikodi.
Hayo yalielezwa jana na Kamishna wa Kodi za Ndani, Alfredy Mregi, wakati wa mafunzo ya mfumo huo kwa walipakodi wa ndani yaliyofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.

Pia Kamishna huyo alisema kwamba kuanzia Februari 9, 2026, makampuni au taasisi 60 zitaanza kuingizwa katika mfumo huo, ambao unatajwa kurahisisha shughuli za kikodi baina ya TRA na wadau wa kodi za ndani, hususan wafanyabiashara wadogo na wakubwa.
“Niseme tu kwamba mfumo huu umekuja wakati muafaka kwa ajili ya kutatua kero na changamoto za muda mrefu kwa wafanyabiashara wetu wa ndani, hivyo utasaidia kupunguza gharama ambazo zilikuwa zikitumika kwa mlipakodi kuja ofisini na wakati mwingine kwa TRA kuwafuata huko waliko. Lingine ni upotevu wa muda na usahihi wake, kwa kuwa kila kitu kimewekwa kwenye mfumo,” alisema Mregi.

Aidha, Mregi alisema mfumo huo utaleta tija kwa wadau wa kodi na TRA kwa kuwa mfumo huo ni rafiki kwa matumizi na si wa gharama, na hivyo kuwaomba wafanyabiashara wajifunze vyema na wauelewe, kwa kuwa una manufaa makubwa, ambapo makampuni na taasisi mbalimbali zitaunganishwa na makadirio ya kodi yatakuwa sahihi pasipo uonevu wowote.
Kwa upande wake, Mwakilishi wa Mwenyekiti wa wafanyabiashara Kariakoo, Pendo Lukasi, alisema wanaishukuru TRA kwa mfumo huo utakaowarahisishia kazi, kwani kwa maelezo ya mafunzo hayo ni mfumo rafiki, alisema Pendo.
“Mfumo huu ni rafiki kwetu; tutawashawishi wafanyabiashara wenzetu kuutumia mfumo huu, kwani umekuja kutatua kilio chetu,” alisema Pendo.
Mfumo huu umeunganishwa na mifumo ya taasisi nyingine za Serikali ili kurahisisha ubadilishanaji wa taarifa na hivyo kuboresha utoaji wa huduma kwa walipakodi na wadau wengine. Mfumo huu unatarajiwa kuanza kutumika rasmi kuanzia mwezi Januari 2026. Mfumo wa IDRAS utamwezesha mtumiaji kujihudumia mwenyewe (self-service) akiwa mahali popote na wakati wowote kwa kutumia Namba ya Utambulisho wa Mlipakodi (TIN).








