

Vikundi vya kijamii vinavyojihusisha na amana ya fedha na kukopeshana (VIKOBA) vimetakiwa kuwa na Mkaguzi wa Ndani wa Fedha ambaye atakuwa akikagua mwenendo wa mahesabu ya vikundi hivyo. Kwa mujibu wa sheria, VIKOBA ambavyo havitakuwa na Mkaguzi wa Ndani vitakuwa vinakiuka sheria na vinapaswa kuchukuliwa hatua kwa kupigwa faini ya kati ya milioni 1 hadi milioni 5.
Akizungumza na waandishi wa habari wanaoshiriki semina ya siku ya pili iliyoandaliwa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mkoani Dodoma, Meneja Usimamizi wa Watoa Huduma Ndogo za Fedha, Dickson Gama, ameviagiza vikundi hivyo kufanya shughuli zake kwa kufuata sheria, vinginevyo vitachukuliwa hatua endapo vitafanya makosa. Majukumu ya Mkaguzi wa Ndani, ambaye anaweza kuwa miongoni mwa wanachama mwenye elimu ya ukaguzi, ni pamoja na kusimamia mikopo inayotolewa na kikundi, kusimamia mfumo wa utunzaji wa fedha za kikundi na kumsimamia mweka hazina kutimiza majukumu yake kwa weledi.
Aidha, Gama amesema kuendesha VIKOBA bila kuvisajili ni kinyume cha sheria, hivyo amewataka wenye vikundi kuvisajili; vinginevyo, vikibainika, vitapigwa faini ya kati ya milioni 10 hadi milioni 50.








