
Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Rogers Shemwelekwa, ametoa wito kwa wananchi wa Manispaa hiyo kuhakikisha wanatunza miundombinu na miradi ya maendeleo inayotekelezwa katika maeneo yao ili kuendana na kasi ya maendeleo ya serikali.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kukagua miradi ya maendeleo katika Kata ya Mbwawa, Dkt. Shemwelekwa alisisitiza umuhimu wa wananchi kushiriki kikamilifu katika kuilinda na kuitunza miradi hiyo kwa manufaa ya wote.

“Haipendezi kuona serikali inatoa fedha nyingi kutekeleza miradi ya maendeleo lakini wananchi hawatunzi miundombinu hiyo,” alisema Dkt. Shemwelekwa. “Kwa mfano, Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha imetoa shilingi milioni 420 kwa ajili ya kutengeneza barabara zenye lengo la kuboresha huduma kwa wananchi, lakini changamoto kubwa imekuwa wananchi kutokutunza barabara hizo mara baada ya kufunguliwa.”
Aliongeza kuwa ni muhimu wananchi watambue kuwa miradi ya serikali ni matokeo ya kodi zao, hivyo wana wajibu wa kuilinda ili idumu kwa muda mrefu.

“Kama leo tumefungua barabara, basi mwaka ujao tuweke kifusi na kuendelea kuboresha zaidi ili tuendelee kupiga hatua za kimaendeleo,” alisisitiza.
Kwa upande wao, wananchi wa Kata ya Mbwawa walimpongeza Dkt. Shemwelekwa kwa uongozi wake makini na kasi ya kusimamia maendeleo, wakibainisha kuwa amekuwa mstari wa mbele kutatua changamoto zinazowakabili. Wameahidi kuendelea kumpa ushirikiano ili kuhakikisha miradi yote ya maendeleo inafanikiwa na kuleta manufaa kwa jamii.








