Home Kitaifa SENDIGA AZINDUA MRADI WA USAMBAZAJI NA UUZAJI WA MAJIKO BANIFU KWA BEI...

SENDIGA AZINDUA MRADI WA USAMBAZAJI NA UUZAJI WA MAJIKO BANIFU KWA BEI YA RUZUKU MANYARA

Mkuu wa Mkoa wa Manyara, Mheshimiwa Queen Sendiga, leo Novemba 10, 2025, amezindua rasmi mradi wa uuzaji na usambazaji wa majiko banifu kwa bei ya ruzuku mkoani Manyara. Uzinduzi huu ni sehemu ya utekelezaji wa mkakati wa kitaifa wa upatikanaji na uhamasishaji wa matumizi ya nishati safi na salama ya kupikia.

Aidha, uzinduzi huu umefanyika katika Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Manyara iliyopo wilaya ya Babati, ambapo jumla ya majiko banifu 7,914 yatauzwa na kusambazwa kwa bei ya ruzuku ya kiasi cha TZS 11,200, ambayo ni sawa na asilimia 80 ya ruzuku ya TZS 56,000, ambayo ni bei ya awali ya jiko.

Akizungumza wakati wa uzinduzi, Mheshimiwa Sendiga amesema mpango huo umelenga kuhakikisha wananchi wote, hususan wa kipato cha chini, wanapata fursa ya kutumia nishati safi na salama ya kupikia kwa gharama nafuu.

Aidha, amewaagiza Wakuu wa Wilaya wote mkoani Manyara kusimamia kwa makini zoezi hili ili kuhakikisha majiko hayo yanauzwa kwa bei iliyoelekezwa na kuepuka udanganyifu wa aina yoyote unaoweza kujitokeza wakati wa zoezi hilo.

Natoa rai kwa Wakuu wa Wilaya wote kuhakikisha taratibu zinazohitajika zinazingatiwa, na majiko haya yanawafikia walengwa kwa bei ya TZS 11,200 kama ilivyoelekezwa. Hatutavumilia udanganyifu na ubadhirifu wowote utakaojitokeza wakati wa zoezi,” amesema Sendiga.

Mheshimiwa Sendiga ameeleza kuwa kampeni hii ni sehemu ya juhudi za Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan za kupunguza uharibifu wa mazingira unaosababishwa na matumizi makubwa ya kuni na mkaa, na pia kulinda afya za wananchi.

Mpango huu wa ruzuku unatarajiwa kuongeza upatikanaji wa nishati safi, salama na nafuu ya kupikia kwa wananchi, na hivyo kuwa chachu ya mabadiliko kuelekea upishi salama na rafiki kwa mazingira.

Akiwasilisha taarifa ya mradi kwa Mkuu wa Mkoa, Mhandisi wa Miradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini, Ramadhani Mganga, amesema kwa Mkoa wa Manyara mradi unatarajia kugharimu kiasi cha zaidi ya TZS milioni 354.5, kiasi ambacho kitawezesha usambazaji na uuzaji wa majiko banifu 7,914 kwa bei ya ruzuku mkoa mzima.

Mhandisi Mganga amesema wilaya zitakazonufaika na mradi ni wilaya zote tano (5) za Mkoa wa Manyara ambazo ni Kiteto, Mbulu, Simanjiro, Hanang na Babati, ambapo kila wilaya itapata majiko 1,583 isipokuwa wilaya ya Babati ambayo itapata majiko 1,582.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!