
Mgombea ubunge Jimbo la Kisarawe kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Dkt. Selemani Jafo, leo Ijumaa Septemba 26, 2025, amehutubia mamia ya wananchi katika Viwanja vya Kisarawe Sokoni na kueleza mafanikio makubwa yaliyopatikana chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Jafo amesema Dkt. Samia alipoingia madarakani alikuta zaidi ya kata 746 nchini hazina shule za sekondari za kata, lakini leo kila kata ina sekondari yake na shule mpya zaidi ya 360 zimeongezwa.
Aidha, amesema Kisarawe imepiga hatua kubwa katika elimu ambapo shule zenye kidato cha tano na sita zimeongezeka kutoka moja hadi kufikia tano.

Katika sekta ya miundombinu na nishati, Dkt. Jafo amebainisha kukamilika kwa Bwawa la Mwalimu Julius Nyerere ambalo limeongeza uwezo wa nchi kuzalisha umeme kutoka megawati 1,690 hadi 4,000.
Pia amesema, mradi wa reli ya kisasa (SGR) umeshaanza kufanya kazi kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma na ujenzi unaendelea maeneo mengine.
Ameongeza kwa kusema kuwa sekta ya afya nayo imepiga hatua kubwa chini ya uongozi wa Dkt. Samia, ambapo sasa kila Kanda nchini ina hospitali ya Kanda, na Hospitali ya Wilaya ya Kisarawe imejengewa majengo mapya ya kisasa, yakiwemo ya ghorofa, pamoja na kupata madaktari bingwa 13, jambo lililoifanya kuwa kituo cha umahiri (center of excellence).

Kwa upande wa huduma za afya, Dkt. Jafo ameema Kisarawe sasa inaongoza mkoa wa Pwani kwa kuwa na vituo vya afya saba, huku kituo cha nane kikiwa kwenye hatua za ujenzi na cha tisa kikitarajiwa kujengwa.
Aidha, ameeleza kuwa vijiji vyote vya Kisarawe tayari vimepata umeme, na hatua inayofuata ni kuhakikisha vitongoji vyote vinapata huduma hiyo.

Ametaja pia miradi mipya itakayotekelezwa, ikiwemo ujenzi wa barabara ya Sungwi–Msangachale yenye urefu wa kilomita 34.5, shule ya msingi ya mchepuo wa Kiingereza mjini Kisarawe, na ujenzi wa shule pamoja na zahanati katika kijiji cha Kimani.
“Ndani ya miaka minne tu ya uongozi wake, Dkt. Samia ametufanyia mambo makubwa ambayo kwa kweli ni miujiza. Naomba tumpe kura zote za ndiyo ili aendelee kuleta maendeleo katika nchi yetu,” alisema Dkt. Jafo.