Na Mwandishi Wetu
Katika msimu mpya wa mashindano ya mpira wa miguu kwa vijana kutoka mitaani, maarufu kama NDONDO CUP, kampuni ya mawasiliano ya YAS imetangaza kuwa mdhamini rasmi wa toleo la mwaka 2025. Hatua hii imepokelewa kwa hamasa kubwa kutoka kwa wadau wa michezo nchini.

Robert Kasulwa, Mkurugenzi wa YAS Kanda ya Dar es Salaam Kusini, amesema kuwa udhamini huo ni sehemu ya mwendelezo wa kampeni ya kampuni hiyo iitwayo “ANZIA ULIPO”, inayolenga kuhamasisha vijana kutafuta mafanikio kuanzia walipo — mitaani, mashinani na bila kisingizio.
“Tunawaamini vijana hawa. Tunaamini kuwa kupitia teknolojia yetu ya kisasa, kama vile huduma za intaneti yenye kasi ya 4G na 5G, tunaweza kuwapa nguvu ya kufikia ndoto zao. Ndondo Cup ni jukwaa halisi la vipaji halisi” – alisema Kasulwa.

Kwa sasa, zimesalia timu 32 katika hatua za mtoano za Ndondo Cup, na ushindani unazidi kupamba moto. Kwa mara ya kwanza katika historia ya mashindano haya, mshindi wa kwanza atazawadiwa kiasi kikubwa cha shilingi milioni 30 — donge nono ambalo limevuka zawadi za miaka ya nyuma kwa mbali.
Waandaaji wa Ndondo Cup wamesema kwamba udhamini huu kutoka YAS si tu unaleta thamani ya kifedha, bali pia unachochea matumaini na morali kwa vijana waliokuwa wakisahaulika, sasa kupata nafasi ya kuonekana kitaifa na hata kimataifa.
 
            
