
Zaidi ya shilingi milioni mia tatu zimetumika kununua vifaa tiba na vifaa vya elimu, ikiwemo madawati zaidi ya elfu tatu pamoja na kompyuta, katika shule za msingi wilaya za Serengeti na Bunda mkoani Mara, ambavyo vimetolewa na Shirika la Grumeti Reserves Limited kwa kushirikiana na TAWA, huku wananchi wakionywa kuacha kujihusisha na shughuli za ujangili kwenye maeneo ya uhifadhi.

Vifaa hivyo vimetolewa kufuatia jamii kushiriki katika uhifadhi wa mazingira na wanyamapori katika mapori ya akiba ya Ikorongo na Grumeti kupitia mfuko wa uhifadhi mahiri SWICA, na sasa shule za msingi katika wilaya za Serengeti pamoja na Bunda zimepokea vitanda, madawati, kompyuta na UPC ambazo zinapelekwa katika maeneo lengwa.
Akizungumza wakati wa kukabidhi vifaa hivyo vya elimu na afya, Mwenyekiti wa Kamati ya Uhifadhi Jamii Mahiri kwa niaba ya Mkurugenzi Mkuu wa Grumeti Reserves Limited alisema msaada uliotolewa ni pamoja na madawati 3,014, vitanda 16 kwa ajili ya kujifungulia, kompyuta 19 pamoja na uwekaji wa maji kwa shule moja ya msingi.

“Tumetoa madawati 1,534 kwa wilaya ya Bunda na 1,480 kwa ajili ya wilaya ya Serengeti, vitanda 12 na vingine vinne kwa ajili ya wilaya ya Serengeti pamoja na vifaa vya TEHAMA kwa wilaya zote,” alisema Frida Mollel.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Angelina Marco, amesema matunda ya uhifadhi yana mchango mkubwa katika maendeleo ya nchi huku akiwataka wananchi kushiriki katika uhifadhi. Sambamba naye, Mkuu wa Wilaya ya Bunda aliwataka wananchi kuhakikisha wanaachana na vitendo vya ujangili katika maeneo yao.








