Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Zanzibar, Abeida Rashidi Abdallah, amesema wanaamini ziara yao ya mafunzo katika shirika la Kivulini lililoko Jijini Mwanza, itakuwa na tija kubwa kwani watapata mbinu za kipekee kutoka kwa shirika hilo.
Akizungumza baada ya mafunzo kuhusu kutokomeza ukatili kwa wanawake na watoto, baadhi ya washiriki wa ziara hiyo wamesema shirika la Kivulini lina uzoefu mkubwa katika kupambana na vitendo vya ukatili.
Aidha, wameongeza kuwa licha ya Serikali ya Zanzibar kuendelea na kampeni mbalimbali visiwani humo, Serikali imeona ni vyema kupata mbinu zaidi kutoka kwa shirika la Kivulini, ambazo zitawasaidia zaidi katika kutokomeza vitendo hivyo.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shirika la Kivulini, Yassin Ally, amesema ziara ya Katibu Mkuu na timu yake itawawezesha kujifunza mbinu mbalimbali za kupambana na ukatili, pamoja na kujifunza jinsi jamii na makundi mbalimbali wanavyoshiriki katika kupinga ukatili.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Wazee ataongoza ziara ya kikazi ya siku tatu mkoani Mwanza.