
Mbunge wa Viti Maalum, JaneJelly James Ntate, ametoa wito kwa serikali kuhusu maendeleo ya miundombinu na sekta za uchumi katika Bunge la 12, Mkutano wa 18, Kikao cha Nne, jijini Dodoma, Februari 6, 2025. Katika mchango wake, Ntate amesisitiza umuhimu wa kuboresha barabara ya Liganga na Mchuchuma, huku akieleza kuwa Rais Samia Suluhu Hassan anafanya jitihada kubwa kumaliza changamoto hiyo.
Ntate ameangazia sekta muhimu za kilimo, viwanda, biashara, uvuvi, na mifugo, akiziomba wizara husika kushirikiana, kwa kuwa sekta hizo ni mhimili wa uchumi wa Tanzania. Ameiomba serikali kufuta madeni ya Taasisi ya SIDO, kuchakata upya sheria za kodi, na kuondoa malipo ya pango la ardhi kwa taasisi za serikali zisizofanya biashara.
Aidha, amesisitiza kuwa serikali inapaswa kuwaamini wazawa kwa kununua bidhaa zao na kuwekeza kwenye vifaa vya kisasa kwenye maabara ya kitaifa ya uvuvi. Katika hatua nyingine, Ntate ameeleza kwamba Tanzania imeshika nafasi ya pili kwa uzalishaji wa mahindi, ikiwa ni ishara ya ukuaji wa sekta ya kilimo. Amepongeza Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo, kwa juhudi za kuendeleza sekta hiyo ipasavyo.