Home Kitaifa WHI YAONGEZA FURSA ZA UWEKEZAJI NA UMILIKI WA NYUMBA

WHI YAONGEZA FURSA ZA UWEKEZAJI NA UMILIKI WA NYUMBA

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Ikulu) anayesimamia Fedha na Mipango Zanzibar, Mhe. Dkt. Saada Mkuya Salum, ametembelea banda la Watumishi Housing Investments (WHI) lililopo katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC), wakati wa Mkutano Mkuu wa Mwaka wa Wakaguzi wa Ndani unaofanyika jijini Arusha kuanzia tarehe 21 hadi 25 Septemba, 2026.

Akiwa katika banda la WHI, Mhe. Dkt. Saada alipata maelezo kuhusu huduma na fursa mbalimbali zinazotolewa na taasisi hiyo, ikiwemo uwekezaji kupitia Faida Fund, huduma ya e-Wekeza pamoja na fursa mbalimbali za kumiliki nyumba. Aidha, alipata nafasi ya kufahamu baadhi ya miradi ambayo WHI imeisimamia na kuitekeleza katika nafasi yake kama Mshauri Elekezi na Mkandarasi wa Ujenzi Daraja la Kwanza.

Baada ya kupokea maelezo hayo, Mhe. Dkt. Saada aliipongeza WHI kwa kazi nzuri inayofanya, huku akisisitiza umuhimu wa taasisi kuendelea kuongeza juhudi za kujitangaza na kutoa elimu kwa umma ili huduma na fursa hizo ziweze kuwafikia wananchi wengi zaidi.

Alisisitiza zaidi umuhimu wa wananchi kuendelea kufikiwa na elimu kuhusu fursa za uwekezaji, hususan kupitia Faida Fund, ili waweze kufahamu namna wanavyoweza kuwekeza na kunufaika na fursa zilizopo.

WHI inaendelea kutumia majukwaa mbalimbali kuwafikia wananchi, kutoa elimu kuhusu huduma zake na kutangaza fursa za uwekezaji, umiliki wa nyumba pamoja na huduma zake za ujenzi na ushauri elekezi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!