
Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene, amewataka wananchi kutokushabikia au kujiingiza katika maandamano yanayodaiwa kwamba yamepangwa kufanyika tarehe 9 Desemba, akibainisha kuwa hayajakidhi matakwa ya sheria na hivyo hayakubaliki.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam leo, Desemba 8, Simbachawene alisema serikali imeimarisha hatua za usalama kufuatia taarifa zinazosambaa kuhusu uwezekano wa kuwepo kwa maandamano yasiyoratibiwa. Alisisitiza kuwa lengo ni kulinda amani na utulivu uliopo nchini.
Amesema kwa sasa hali ya nchi iko shwari, lakini vyombo vya usalama vinaendelea kufuatilia kwa ukaribu taarifa zote zinazoashiria mipango ya maandamano. Alionya kuwa hatua yoyote inayoweza kusababisha uvunjifu wa amani haitavumiliwa.
“Maandamano hayo hayana mwombaji, hayaelezi yanatoka wapi kwenda wapi, wala ujumbe wake ni nini. Yanaelezwa kuwa hayana ukomo na yanadaiwa kuwa makubwa kuliko yale ya tarehe 29. Hayo si maandamano, ni mapinduzi, na tutayadhibiti,” alisema Simbachawene.
Waziri huyo alifafanua kuwa taarifa za aina hiyo, kwa mujibu wa sheria, ni tishio kwa usalama wa umma, na ndiyo sababu serikali imechukua hatua za mapema kuhakikisha usalama wa raia na mali zao unaendelea kuwepo.
Serikali imetoa wito kwa wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya dola katika kudumisha utulivu. “Tunawaomba wananchi mtujulishe mara mnapohisi kuna viashiria vya mipango ya kutekeleza maandamano hayo ya tarehe 9,” alisema.
Hadi sasa, hakuna kikundi au mtu aliyethibitishwa kujitokeza kupanga au kudai kuandaa maandamano hayo, na hivyo vyombo vya usalama vimeelekezwa kuyadhibiti endapo yatajaribu kufanyika.








