
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ameielekeza Mamlaka ya Maji Safi na Maji Taka (DAWASA) kuhakikisha kuwa maji yanayopatikana yanatumika kwa mahitaji ya binadamu pekee katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, kufuatia changamoto ya upungufu wa maji inayoendelea kujitokeza.

Akizungumza na waandishi wa habari Desemba 10, 2025, mara baada ya ziara ya ukaguzi katika chanzo cha uzalishaji cha Ruvu Juu, Waziri Aweso ameeleza kuwa serikali inaendelea kufanya jitihada za kuhakikisha wananchi wanapata huduma ya maji, na ameongeza kuwa ni muhimu kwa wananchi kutunza na kuhifadhi maji.
“Kwa sasa maji haya yote yawe kipaumbele kwa matumizi ya binadamu. Kiwango kilichopo kigawiwe kwa usawa,” Aweso ameongeza. Aidha, amesema ni lazima kujenga utamaduni wa kuhifadhi maji ili kukabiliana na vipindi vya upungufu wa huduma hiyo.
Waziri Aweso ameendelea kuwaomba wakazi wa Dar es Salaam na Pwani kuwa wavumilivu, akibainisha kuwa kipindi hiki ni cha mpito na kwamba mvua zinazoanza kunyesha zitaongeza maji katika vyanzo na kurejesha upatikanaji wa huduma katika kiwango cha kawaida.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Bodi ya Maji Bonde la Wami–Ruvu, Elibariki Mmasi, amesema taasisi hiyo imechukua hatua ya kurejesha maji yaliyokuwa yanapotea katika Mto Ruvu kwenye mkondo mmoja, hatua iliyoongeza kiwango cha maji katika mto.
Mmasi amesema wamekagua vyanzo vya maji na kusitisha shughuli zote zisizo za matumizi ya majumbani ambazo zilikuwa zikisababisha kupungua kwa maji. Amefafanua kuwa doria inaendelea kufanyika katika maeneo yote na kiwango cha maji kimeanza kuongezeka.
“Tunaamini kwamba katika kipindi kifupi, hali ya matumizi ya maji itarejea katika utaratibu wa kawaida,” Mmasi ameongeza.








