Wanawake wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) mkoa wa Dodoma leo Machi 8, 2026 wameungana na wanawake wenzao wa mkoa wa Dodoma, Tanzania na ulimwenguni kuadhimisha Siku ya Mwanamke Duniani, ambapo maadhimisho ya kimkoa yamefanyika katika wilaya ya Kongwa.
Maadhimisho hayo yalipambwa na shamrashamra mbalimbali zikiwemo burudani za ngoma za asili, matarumbeta pamoja na Brass Band ya JKT Makutupora. Mgeni rasmi katika hafla hiyo alikuwa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Mhe. Rosemary Senyamule.
Mapema asubuhi ya leo, wanawake walikusanyika katika viwanja vya maadhimisho kabla ya kuanza kwa maandamano rasmi. Walionekana kuwa na uchangamfu na kujiamini, hali iliyoonesha ari kubwa ya kushiriki katika maadhimisho hayo muhimu.
Baadhi ya wanawake wa TBA waliozungumza katika maadhimisho hayo wamesema kuwa maadhimisho ya mwaka huu yamekuwa ya kuvutia na yenye kuhamasisha ushiriki wa wanawake katika nyanja mbalimbali za maendeleo.
Akizungumzia maendeleo ya wanawake ndani ya TBA, Afisa Rasilimali Watu wa TBA, Bi. Nashila Iddi amesema kuwa wanawake ndani ya taasisi wamepiga hatua kubwa kitaaluma na kiutendaji.
Amesema kuwa idadi ya wanawake wataalamu kama wahandisi, wakadiriaji majengo (QS) pamoja na wabunifu wa majengo inaendelea kuongezeka kila mwaka, jambo linaloonesha maendeleo chanya katika ushiriki wa wanawake katika taaluma za ujenzi.
“Ndani ya TBA tuna wanawake wengi katika nafasi za uongozi. Yupo Mkurugenzi, wapo mameneja wa mikoa, wakuu wa vitengo pamoja na wasimamizi wa miradi, na wote wanafanya kazi zao kwa ufanisi mkubwa,” amesema Bi. Nashila.
Kwa upande wake, Afisa Manunuzi wa TBA, Bi. Ruth Mwakalinga amesema wanawake wanazidi kujiamini kadri wanavyopata fursa katika maeneo mbalimbali ya kazi.
“Wanawake wanazidi kujiamini kila mwaka, na kila wanapopata nafasi wanaonyesha uwezo mkubwa walionao katika kuleta maendeleo,” amesema.
Naye Maria Paulo, ambaye anafanya kazi katika mradi wa ujenzi wa nyumba 3,500 unaotekelezwa na TBA katika eneo la Nzuguni, amesema wanawake kwa sasa wanajituma zaidi katika utekelezaji wa miradi.
“Wanawake kwa sasa wanajituma sana. Hata hapa kwenye mradi wetu tunaona namna wanavyofanya kazi kwa bidii na kujituma,” amesema.
Siku ya Mwanamke Duniani huadhimishwa kila mwaka Machi 8 ikiwa na ujumbe maalum wa kuhamasisha haki, usawa na maendeleo ya wanawake. Kaulimbiu ya mwaka huu inasema: “Haki na Usawa kwa Wanawake na Wasichana ni Msingi Jumuishi wa Kufikia Dira ya Maendeleo 2050.”












