Home Kitaifa WANANCHI VUO WAPATIWA FEDHA KUNUSURU RASILIMALI BAHARI

WANANCHI VUO WAPATIWA FEDHA KUNUSURU RASILIMALI BAHARI

Na Boniface Gideon, TANGA

Wakazi wa kijiji cha Vuo wilayani Mkinga mkoani Tanga, wamepatiwa mafunzo ya usimamizi wa mazingira ya bahari na usimamizi wa fedha ikiwa ni juhudi za kunusuru viumbe baharini ikiwemo makazi ya samaki (matumbawe), kulinda uvuvi haramu, kutunza fukwe, upandaji miti ya mikoko pamoja na kulima kilimo cha mwani.

Sambamba na mafunzo hayo, wakazi wamepatiwa fedha Sh. 10.5 mil. kwa ajili ya kuendesha biashara ili kupunguza utegemezi wa shughuli za baharini.

Fedha hizo ni sehemu ya mradi wa ‘Pwani Yetu’ unaosimamiwa na Shirika la Maendeleo la GIZ kwa kushirikiana na Shirika la Mwambao Coastal Community Network Tanzania.

Akizungumza jana, wakati wa hafla ya kukabidhi fedha kwa wakazi wa kijiji hicho, Mratibu wa Mipango kutoka Shirika la Mwambao Coastal Community Network Tanzania, Abubakar Masoud, alisema fedha hizo zimetolewa kwenye vikundi 5 vyenye wanachama 150, kwa ajili ya kuwasaidia kujikwamua kiuchumi kupitia biashara ili kupunguza utegemezi wa shughuli za kibinadamu baharini.

Fedha hizi ni sehemu ya mkakati wetu wa kupunguza shughuli za kibinadamu baharini na kuongeza kipato kwa wakazi. Tunatarajia kuona matokeo chanya ya fedha hizi. Niwaombe watu wote mnaokwenda kunufaika na fedha hizi mkazitumie kwenye malengo yaliyokusudiwa ili yate matokeo chanya yaliyokusudiwa,” alisisitiza Masoud.

Kwa upande wake, Mratibu wa Shirika la Mwambao Coastal Community Network Tanzania mkoa wa Tanga, Ahmad Salim, alisema kabla ya kutolewa kwa fedha hizo, wakazi wa kijiji hicho walipatiwa mafunzo maalumu ya kuwajengea uwezo kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo utunzaji wa mazingira na usimamizi wa fedha.

Kabla ya hatujatoa fedha hizi, tulianza kuwajengea uwezo wa kiuchumi, usimamizi wa mazingira na fedha. Lengo ni kuwafanya wakazi hawa waweze kujisimamia hata sisi tukiwa hatupo. Tunaamini elimu waliyoipata itawasaidia kusimamia utunzaji wa mazingira na fedha, na kila mmoja atakuwa balozi wa mazingira. Hivyo niwaombe kila aliyepata elimu hii akawe balozi wa mazingira ili tutimize lengo,” aliongeza Ahmad.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!