Home Kitaifa WALIPAKODI WATAKIWA KUMALIZA MWAKA BILA MADENI YA KODI

WALIPAKODI WATAKIWA KUMALIZA MWAKA BILA MADENI YA KODI

Walipakodi nchini wametakiwa kutimiza wajibu wao wa kulipa kodi ya mapato awamu ya nne na kuwasilisha ritani za kodi ya ongezeko la thamani kwa wakati ili wamalize mwaka 2025 bila madeni ya kodi hali ambayo itawaepushia riba na adhabu.

Rai hiyo imetolewa Desemba 12.2025 na Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Bw. Yusuph Juma Mwenda alipokutana na kufanya mazungumzo na Mawakala wa Forodha na Washauri wa Kodi Jijini Dar es Salaam.

Akizungumza katika kikao hicho Kamishna Mkuu amesema kila mmoja anao wajibu wa kulipa kodi na kuisaidia nchi kujitegemea kwa mapato kwa kulipa kodi kwa wakati na kwa hiari.

Kamishna Mkuu amesema Washauri wa Kodi na Mawakala wa Forodha wanaowajibu wa kuwahimiza walipakodi wanaowahudumia kufuata sheria na kuwashauri kutokukwepa kodi kwani wakibainika watakutana na mkono wa sheria.

Tunajua upo ukwepaji kodi unaofanyika kwa namna mbalimbali ikiwemo kufanya magendo, kutokutoa risiti za mauzo, kufanya makadirio ya uongo na njia nyingine nyingi ambazo mnazijua hivyo tunawaomba muisaidie nchi kwa kufichua ukwepaji kodi” amesema Mwenda.

Amesema vutendo vya ukwepaji kodi vinapunguza ushindani wa biashara sokoni na imani ya walipakodi wazuri hivyo hali ambayo inaendelea kupunguza wigo wa kodi.

Amesema TRA imejipanga kuongeza wigo wa kodi kwa kuongeza mapambano dhidi ya wakwepaji wa kodi na kuzuia kufanyika kwa magendo.

Kwa upande wake Rais wa Chama cha Mawakala wa Forodha (TAFFA) Bw. Edward Urio ametoa wito kwa walipakodi kufuata sheria za kodi kwa kutimiza wajibu wao wa kukamilisha mwaka wa kalenda bila madeni ya kodi na kuipongeza TRA kwa kuendelea kuboresha huduma kwa Walipakodi.

Urio amesema kwa Mawakala wa Forodha majukumu yao yamerahisishwa kupitia mfumo wa TANCIS ulioboreshwa ambao umekuwa ukiwarahisishia uondoshaji wa mizigo kutokana na kufanya taratibu zote kupitia mtandao.

Naye mwakilishi wa Washauri wa Kodi Bi. Victoria Soka amesema wao kama Washauri wa Kodi watakwenda kutimiza wajibu wao kwa kuwashauri wateja wanaowahudumia watimize wajibu wao kwa wakati ili kuisaidia nchi kujitegemea.

Amesema wao wamekuwa wakijenga utamaduni wa kulipa kodi kwa wanafunzi wa shule za msingi kwa kuwapatia Elimu ya kodi shuleni lengo likiwa ni kuwawezesha watoto kukua wakitambua umuhimu wa kulipa kodi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!