
Wadau wa uhifadhi na utalii katika mikoa ya nyanda za juu kusini wamehamasishwa kushiriki katika tuzo za uhifadhi na utalii za Serengeti (Serengeti Awards 2025) zinazotarajiwa kufanyika mwezi Desemba 2025.
Mkurugenzi Msaidizi, Idara ya Utalii, Bi. Dainess Kunzugala amesema hayo leo katika kikao na wadau hao wakiwemo makampuni na waendeshaji wa shughuli za utalii , waongoza watalii , watoa huduma za malazi , wahifadhi na mashirika au taasisi zenye mchango katika uhifadhi kilichofanyika Novemba 17, 2025 Mkoani Iringa.

“Natoa hamasa kwa wadau wetu wa utalii kutumia fursa hii muhimu kutuma maombi yao kuwania tuzo hizi muhimu ambapo kuna kategoria zipatazo saba ambazo zimeainisha makundi mbalimbali” amesema Bi. Kunzugala.
Amesema lengo ni kutambua mchango wa wadau hao pamoja na kuifanya sekta ya utalii iwe na mwamko katika kuleta maendeleo nchini.
Naye, Mwongoza Watalii kutoka kampuni ya Mukuta Travel and Tours, Bw.Fadhili Laizer ameishukuru Wizara ya Maliasili na Utalii kwa elimu ya namna ya kujisajili na kuwania tuzo hizo.
“Wadau wa utalii nyanda za juu kusini na maeneo mengine niwaambie tu ni vyema wakajitokeza kwa wingi kushirikiana kuwania tuzo hizo ili kukuza utalii lakini pia kujitangaza zaidi” amesema Bw. Fadhili.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Iringa Tourism Association ,Bw.Serafina Lanz ameishauri Serikali kufikiria kuendeleza mikoa ya nyanda za juu kusini ambayo ina hifadhi kubwa kama Nyerere , Ruaha na kupendekeza tuzo zijazo ziitwe majina kama Nyerere Awards au Ruaha Awards.








