
Naibu Waziri wa Nishati, Salome Makamba, ameielekeza Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na Mamlaka ya Udhibiti wa Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) kuhakikisha Watanzania wananufaika moja kwa moja na rasilimali za mafuta na gesi, hususan katika upatikanaji wa ajira, huduma za kijamii na nishati nafuu.

Akizungumza leo Desemba 08, 2025 jijini Dar es Salaam, wakati wa ziara aliyoifanya katika taasisi hizo baada ya kuteuliwa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, Salome aliitaka Menejimenti ya TPDC kuongeza kasi ya usambazaji wa gesi majumbani ili kuimarisha upatikanaji wa nishati hiyo muhimu kwa wananchi wengi zaidi, sambamba na kuhakikisha matokeo ya miradi yanaonekana na kuleta tija kwa Taifa.

Aidha, aliipongeza TPDC pamoja na PURA kwa jitihada wanazoendelea kufanya katika utafiti, uendelezaji na usimamizi wa sekta ya mafuta na gesi asilia, huku akizisisitiza kuendelea kuboresha mazingira rafiki ya uwekezaji kwa lengo la kuchochea ajira na kuongeza manufaa kwa wananchi.
Waziri Salome alisisitiza umuhimu wa miradi ya utafiti na uendelezaji wa gesi asilia, ikiwemo mradi wa LNG, kupewa kipaumbele ili kuongeza tija ya uzalishaji na kuhakikisha nchi inanufaika kikamilifu na rasilimali zake. Pia aliongeza kuwa taasisi zote zilizo chini ya wizara zinapaswa kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa maagizo ya Serikali kuhusu usimamizi wa gesi asilia.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati, Dkt. James Mataragio, aliitaka TPDC kuongeza uzalishaji na upatikanaji wa gesi ili iweze kuwafikia wananchi kwa wingi, huku akiisisitiza PURA kuwapa wawekezaji kipaumbele katika miradi ya mafuta na gesi kwa lengo la kuongeza mapato ya Serikali na maslahi kwa wananchi.
Mkurugenzi Mtendaji wa TPDC, Mussa Makame, alisema shirika linaendelea kuimarisha miundombinu ya uhifadhi na usafirishaji wa mafuta na gesi pamoja na kupanua miradi ya gesi ikiwemo LNG. Naye Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Eng. Charles Sangweni, alisema PURA itaendelea kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi ili kufanikisha malengo ya sekta kwa mujibu wa Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.








