Home Kitaifa TANZANIA YAUZA BIDHAA ZA DOLA MILIONI 22 NCHINI SAUDI ARABIA – LONDO

TANZANIA YAUZA BIDHAA ZA DOLA MILIONI 22 NCHINI SAUDI ARABIA – LONDO

📌 Ni kupitia ushirikiano wa kibiashara baina ya pande hizi mbili;

📌 Naibu Waziri Londo ashiriki maadhimisho ya miaka 96 ya Taifa la Saudi Arabia kama mgeni rasmi;

📌 Balozi wa Saudi Arabia ampongeza Rais kwa kudumisha ushirikiano baina ya nchi hizi mbili.

Na. Neema Chalila Mbuja

Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Dennis Londo, amesema Tanzania imefanikiwa kuuza bidhaa zenye thamani ya takribani dola milioni 22 nchini Saudi Arabia kutokana na ushirikiano wa kibiashara uliopo kati ya Tanzania na Saudi Arabia.

Mhe. Londo ameyasema hayo wakati wa hafla ya kusherehekea miaka 96 ya Taifa la Saudi Arabia, ambapo alikuwa mgeni rasmi. Hafla hiyo ilihudhuriwa na mabalozi na wawakilishi mbalimbali wa makampuni ya kimataifa.

Amesema Tanzania na Saudi Arabia zinaendelea kuimarisha uhusiano wa kihistoria na ushirikiano katika sekta mbalimbali, ikiwemo biashara, elimu na uwekezaji. Ameongeza kuwa uhusiano huo umeendelea kuimarika, huku wigo wa biashara ukiongezeka na Watanzania wengi wakipata fursa za ufadhili wa masomo (scholarships) nchini Saudi Arabia.

Londo amesema Tanzania imekuwa ikiagiza mafuta, bidhaa za petrochemical na mbolea kutoka Saudi Arabia, huku Saudi Arabia ikiagiza nyama na bidhaa za kilimo kutoka Tanzania.

Kwa upande wake, Balozi wa Saudi Arabia nchini Tanzania, Mhe. Yahya bin Ahmed Okaish, amempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kudumisha undugu na urafiki kati ya Tanzania na Saudi Arabia, pamoja na kufungua milango ya biashara baina ya pande hizo mbili.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!