

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Mheshimiwa Antonio Guterres, amesema Tanzania imekuwa ni rejea muhimu ya amani na mshikamano wa kijamii barani Afrika na duniani kote.
Guterres aliyasema hayo leo, tarehe 14 Desemba 2025, wakati akipokea Ujumbe Maalum kutoka Tanzania uliowasilisha salamu na ujumbe wa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Ameeleza kuwa taswira ya Tanzania kama kielelezo cha amani ilijaribiwa katika uchaguzi wa hivi karibuni uliofanyika tarehe 29 Oktoba 2025, ambapo taifa hilo lilikabiliwa na changamoto, lakini liliweza kuvuka mtihani huo kwa mafanikio.
“Umoja wa Mataifa ungependa kuona Tanzania ikiendelea kubaki katika umoja wake na kuwa mfano bora wa amani kwa mataifa mengine,” alisema Katibu Mkuu Guterres.
Ujumbe huo uliwasilishwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mheshimiwa Balozi Mahmoud Kombo, aliyemwakilisha Rais Samia Suluhu Hassan.
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa alisisitiza umuhimu wa kuwepo kwa mazungumzo ya kitaifa yenye maana, jumuishi na shirikishi ili kushughulikia chanzo cha matukio ya vurugu yaliyotokea tarehe 29 Oktoba, pamoja na kutafuta suluhu za kudumu ili kuzuia yasijirudie tena.
Aidha, Guterres aliahidi msaada kamili wa Umoja wa Mataifa kwa Tanzania wakati wote, ikiwemo kipindi cha utekelezaji wa majukumu ya Tume ya Uchunguzi iliyoanzishwa nchini humo na hata baada ya kukamilika kwa kazi zake.








