
Na Shomari Binda-Musoma
SHEIKH wa Wilaya ya Musoma Abubakar Mukama amewahimiza waumini wa dini ya Kiislam kutoa swadaka katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan.
Ujumbe huo ameutoa leo machi 10 ikiwa ni Ramadhan 9 baada ya kumalizika swala ya adhuhur nje ya viwanja vya Msikiti wa Taqwa.
Amesema swadaka ni muhimu katika kuimalisha funga ya mfungaji kwa kutoa ikiwa ni kwa jambo lolote linalotolewa swadaka
Sheikh amesema ipo swadaka ya ujenzi na ukarabati wa misikiti unaoendelea maeneo mbalimbali ya Wilaya ya Musoma na maeneo mengine.
Amesema hakuna swadaka bora kama kuchangia ujenzi wa Msikiti hivyo kila muumini katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan ni vyema kujibidiisha katika kutoa.
Kiongozi huyo wa dini amesema licha ya uchangiaji wa ujenzi wa misikiti kwa kutoa swadaka ni muhimu pia kuwaona wenye uhitaji kwaajili kufuturisha vikiwemo vituo vya watoto yatima,magereza na wahitaji wengine.
“Niwakumbushe ndugu zangu katika imani katika kipindi hiki cha mwezi mtukufu wa Ramadhan licha ya ibada nyingine kujikita pia kwenye utoaji wa swadaka ili kuziweka vizuri swaumu zetu kwa kutoa.
“Kuna misikiti inajengwa kwenye maeneo yetu na wenye uhitaji ambao viongozi wa misikiti wanatufikishia ujumbe tusichoke kutoa kwaajili ya swaumu zetu na kesho akhera”,amesema.
Aidha Sheikh Abubakar amesisitiza kusimamisha swala kwa kila kipindi zikiwemo za faradh na sunna na kudumu hata baada ya funga ya mwezi huu mtukufu wa Ramadhan.
Amesema katika kipindi chake cha uongozi anataka kuona misikiti ya pembezoni ikikarabatiwa na kujengwa na baadae kujengwa Msikiti wa Wilaya.