Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam Mhe. Amos Makalla ametoa wito kwa Bank ya NMB kuendelea kubuni huduma rafiki kwa Makundi mbalimbali katika Jamii ili kuweza kuwafikia Wateja wengi Zaidi.
RC Makalla ametoa wito huo wakati wa Warsha kwa Viongozi wa Serikali wa Mkoa huo iliyolenga kueleza Fursa mbalimbali zinazopatikana katika bank hiyo ikiwemo mikopo ya riba nafuu.
Hata hivyo RC Makalla ametoa wito kwa Halmashauri za Mkoa huo kushirikiana na Bank hiyo hususani kwenye kukopa fedha za kuwezesha kutekeleza miradi yenye Tija na itakayoongeza mapato kwa Halmashauri.
Aidha RC Makalla amepongeza Bank hiyo kwa kutoa Gawio la Shilingi Bilioni 30.7 kwa Serikali pamoja na ushirikiano mkubwa wanaoonyesha kwa Serikali ya Mkoa huo katika kufanikisha masuala ya kijamii ikiwemo Elimu, Afya, Usafi.
Kwa upande wake Mtendaji Mkuu wa Bank hiyo Ruth Zaipuna amesema malengo matano ya kuandaa Warsha hiyo ni pamoja na kuwaeleza faida ya kutumia bank ya NMB, Uwezo wa Bank na utayari wa kufanya Kazi nao, Kutumia Fursa ya Teknolojia na ubunifu wa bank yao katika ukusanyaji mapato na Malipo mbalimbali.
Aidha Zaipuna amesema lengo Lingine ni kuomba Halmashauri kushirikiana na Bank katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo kupitia mikopo ya riba nafuu na Kuwaomba Viongozi hao kuwa mabalozi kwenye kutambulisha bidhaa zao.
Bi. Zaipuna pia amemuhakikishia RC Makalla kuwa bank ya NMB itaendelea kushirikiana na Serikali ya Mkoa huo katika masuala yote ya kijamii.