Home Kitaifa PROF.MKENDA SERIKALI KUJA NA MAGEUZI MAKUBWA YA ELIMU NCHINI

PROF.MKENDA SERIKALI KUJA NA MAGEUZI MAKUBWA YA ELIMU NCHINI

Amesema Serikali kusheherekea Siku ya Mwalimu Duniani 2023 Bukombe

Ahaidi kujenga VETA wilaya ya Bukombe

Imeelezwa kuwa, Serikali imepanga kufanya mageuzi makubwa katika utoaji wa elimu bora hususan katika elimu ya ujuzi wa vitendo katika Sekta ya Elimu nchini.

Hayo yamesemwa na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia Prof. Adolf Mkenda wakati wa Sherehe ya Siku ya Mwalimu Duniani iliyoandaliwa na Chama cha Walimu wa wilaya ya Bukombe Mkoani Geita.

Amesema, walimu wanaandaliwa vizuri katika kuboresha miundombinu ya elimu nchini na kutoa mfano kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kujenga madarasa zaidi ya 600 katika mkoa wa Geita na kuboresha mazingira ya kazi kwa walimu ili kuweka mazingira mazuri ya ufundishaji.

Vile vile, Serikali itaweka mkakati mzuri wa elimu ili kusaidia walimu nchini kuweza kujiendeleza pamoja na kuongeza ujuzi. Ameongeza ndoto ya Serikali ni kuona mwalim anajiendeleza ili aweze kuwa mwalimu bora.

“Mwalimu akiomba ruhusa ya kwenda kusoma mpe ruhusa, mwalimu ni ufunguo wa maisha katika maendeleo ya nchi yetu, mafunzo kazini yataendelea, Serikali ya awamu ya sita imetenga bajeti kwa ajili ya kuwaendeleza walimu,” amesema Prof.Mkenda.

Aidha,Prof Mkenda amemhakikishia Dkt.Biteko kuwa, mwaka 2023 katika kusheherekea Siku ya Mwalimu Duniani Serikali itahakikisha siku hiyo inasheherekewa Kitaifa katika wilaya ya Bukombe ili walimu wakutane kwa pamoja.

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Bukombe na Waziri na Waziri wa Madini Dkt. Doto Biteko amesema mwalimu ni msingi wa elimu na Serikali inautambua mchango wa wao katika utoaji wa elimu.

Pia, amewataka walimu waendelee kushirikiana katika shughuli zao za kila siku, wakipendana, kuthaminiana na kusaidiana wao kwa wao ili kujenga umoja.

Naye, Mkuu wa Mkoa wa Geita Martin Shigela amempongeza mbunge wa Jimbo la Bukombe Dkt. Biteko kwa kuandaa Siku ya Mwalimu Duniani kwa kuadhimishwa katika wilaya ya Bukombe.

Shigela amesema, atahakikisha mwaka 2023 tukio hilo linakuwa kubwa na kuadhimishwa katika Halmashauri nyingine za Mkoa wa Geita ili kusheherekea kwa pamoja.

Siku ya Mwalimu Duniani imeandaliwa na Chama cha Walimu wa wilaya ya Bukombe na imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!