
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan amesema vurugu na uharibifu uliotokea nchini unaweza kuipunguzia sifa Tanzania ya kuweza kupata mikopo na misaada mbalimbali kutoka kwenye Taasisi za Kimataifa, akiwataka Mawaziri kujipanga katika utafutaji wa fedha na matumizi ya rasilimali zilizopo ili kutekeleza miradi ya maendeleo.
Ametoa kauli hiyo leo Novemba 18, 2025 Dk.Samia wakati akiwaapisha Mawaziri na Manaibu Mawaziri wa serikali ya awamu ya Sita Ikulu, Chamwino Mjini Dodoma, alikiri kuwa rasilimali za Taifa ni chache suala ambalo limeifanya Tanzania kuwa tegemezi wa Mikopo kutoka nje.
“Yaliyotokea nchini kwetu yametutia doa kidogo na huenda yakatupunguzia sifa ya kupata hiyo mikopo kwa urahisi kama tulivyopata muhula wa kwanza ambapo tulipata sana kwa sifa zetu, kwa msimamo wetu na kwa kazi tulivyofanya,”amesisitiza.

Amesema Serikali ya Awamu ya Sita inaanza mkakati mpya wa kutekeleza miradi ya kimkakati kwa kutumia fedha za ndani kabla ya kuhusisha washirika wa maendeleo, ili kuongeza kasi ya utekelezaji na kupunguza ucheleweshaji unaotokana na michakato mirefu ya mikopo na misaada kutoka nje ya nchi.
Rais Dk. Samia amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha miradi ya maendeleo nchini inatekelezwa kwa wakati, huku serikali ikiweka mbele maslahi ya wananchi.
“Muhula wa pili wa Serikali ya Awamu ya Sita tutaanza kufanya miradi wenyewe, halafu mashirika yatatukuta njiani kisha tutakwenda nao. Tutaanza kwa fedha za ndani, kisha wakimaliza taratibu zao watatukuta tukiendelea,” amesema.
Aidha amewataka Mawaziri na Manaibu Mawaziri walioapishwa kuongeza kasi na uwajibikaji katika majukumu yao, akisisitiza kuwa muda wa kutekeleza ahadi kwa wananchi ni mchache ukilinganisha na ukubwa wa majukumu yaliyoko mbele.
“Mambo ambayo tumeahidi kwa wananchi ni mengi mno lakini muda wa kuyatekeleza ni mchache. Kwa hiyo wale mlioapa leo mjue tuna kazi ya kwenda mbio, tena mbio haswa,” amesisitiza.
Rais Samia pia amekemea utoaji wa taarifa zisizoonesha matokeo halisi, akibainisha kuwa wananchi wanapaswa kuona athari za kazi za serikali katika maisha yao, si kusikia kauli tu.
“Sitaki zile za ‘tunaendelea’ au ‘mchakato uko mbioni’, nataka impact (matokeo) na matokeo hayo yawe kwa wananchi na si ofisini kwako,”ameongeza.
Amesisitiza kuwa majukumu na dhamana alizotoa kwa Mawaziri na Manaibu mawaziri ni dhamana za kazi na sio fahari, akiahidi kufuatilia mienendo ya wateule hao katika kutimiza kaulimbiu ya serikali yake ya Kazi na utu, tunasonga mbele.
“Dhamana zetu ni dhamana za kazi na si fahari kwamba na mimi ni Waziri ikawa ndio fahari ulipotoka, unapokaa na kwingineko. Tumebeba majukumu ya kwenda kuwatumikia wananchi. Utu uanze na sisi wenyewe Viongozi ambao tunaenda kuwasimamia wengine.
Kwa wale watakaobeba Uwaziri kama fahari, nimeapa leo na mimi nimeukwaa watanijua huko mtaani basi niwaambie tutafuatana polepole, mnaenda lakini tupo nyuma yenu na miaka mitano si midogo lakini si mingi sana kwahiyo mimi sioni shida kubadilisha na mnanijua na kipindi fulani mlishanisema kuwa nabadilisha sana na nikasema ndio nabadilisha mpaka nipate yule ambaye atafanya kazi na mimi kwa moyo Mkuu na kwa moyo mmoja,” amesisitiza Dk. Samia.
Amesema kazi kubwa kuanzia leo kwa wateule hao ni kuwajibika kwa wananchi na kwa Taifa, akisema ahadi kwa wananchi ni nyingi mno na muda wa kutekeleza ni mchache, akiwataka wale wazito wa mwili kupunguza kilo zao ili kuendana na kasi anayoitaka katika kutimiza ahadi zake kwa wananchi.
Aidha Rais Samia pia amewapa pole wateule wake hao kwa kazi nzito iliyo mbele yao, akiwapongeza pia kwa kuaminiwa kuingia katika Baraza la Mawaziri, akiwataka kufanya kazi kwa bidii katika kuwatumikia watanzania.








