
Na Shomari Binda-Musoma
MBUNGE wa Jimbo la Musoma mjini Vedastus Mathayo ameahidi kukamilisha ujenzi wa ofisi ya Chama cha Mapinduzi Kata ya Kigera
Ahadi hiyo ameitoa leo machi 4, 2025 kwenye viwanja vya ofisi hiyo wakati akielezea utekelezaji wa ilani kwenye Mkutano Mkuu wa Kata hiyo.
Amesema viongozi wa chama katika kutekeleza majukumu yao wanapaswa kukaa na kufanya kazi kwenye mazingira mazuri yakiwemo ya ofisi.
Mbunge huyo ambaye anaendelea na ziara yake ya kupita kila Kata kuelezea utekelezaji wa ilani amesema alianza kuijenga ofisi hiyo tangu mwanzo na wanachama kuahidi kuikamilisha lakini kutokana na kukwama ameamua kuikamilisha.
Akizungumzia utekelezaji wa ilani amesema kila mwachama wa CCM anapà swa kutembea kifua mbele kutokana na ahadi nyingi kutekelezwa.

Amesema Kata ya Kigera imekuwa ya kwanza kwenye manispaa ya Musoma kujengwa shule ya ghorofa kwaajili ya wanafunzi wa sekondari.
Mathayo amesema kwenye elimu hakuna tena uhaba wa vyumba vya madarasa na tayari ameleta mbao zaidi ya elfu 30 kwaajili ya utengenezaji wa madawati,meza na viti kwaajili ya wanafunzi na walimu.
” Tumefanya utekelezaji wa ilani ambao kila mmoja amejionea hivyo kila mwanachama anapaswa kutembea kifua mbele na kumsemea vizuri Rais Dkt.Samia Suluhu.
“Na hii ofisi yetu kwa hapa Kigera naona imesimama kwa muda mrefu nipo tayari kuikamilisha ili viongozi wetu wapate mahala pazuri pa kufanya shughuli za chama”,amesema.
Diwani wa Kata ya Kigera Alex Nyabiti amemshukuru mbunge huyo kwa ufatiliaji wake na kupelekea miradi mingi kufika Kata ya Kigera.
Amesema yapo mambo madogo ambayo yanahitaji ukamilishwaji ambayo anaamini kwa kushirikiana na mbunge huyo yanakwenda kukamilishwa.
