
Wananchi wameendelea kunufaika kupitia kampeni ya Kitaifa ya msaada wa kisheria ya Mama Samia Legal Aid, ambapo mfanyakazi wa nyumbani, Anitha Gabriel, hatimaye amepata mishahara yake aliyodhulumiwa kwa miaka minne.
Anitha alikuwa akimdai mwajiri wake zaidi ya shilingi 700,000 baada ya kufanya kazi za ndani jijini Arusha bila kulipwa. Kupitia msaada wa timu ya Mama Samia Legal Aid, ambayo kwa sasa ipo kwenye kampeni ya siku 10 katika Manispaa ya Ilemela, Mwanza, ameweza kurejeshewa sehemu ya haki yake.
Mwenyekiti wa mtaa wa Bugogwa, Jagan Said, na Mwenyekiti wa mtaa wa Igombe, Mathias Mkono, wameshuhudia Anitha akikabidhiwa shilingi 200,000 kama sehemu ya malipo yake. Wamepongeza kampeni hiyo kwa kusaidia wananchi wanyonge na kuwasihi wenye changamoto za kisheria kujitokeza ili kupata haki zao.
Kwa upande wake, Mratibu wa kampeni hiyo Manispaa ya Ilemela, Koku Mwanemile, amesema juhudi zinaendelea kuhakikisha Anitha anapata fedha zake zote kulingana na makubaliano yaliyofikiwa.
Ameongeza kuwa kampeni ya Mama Samia Legal Aid inalenga kuwasaidia wananchi wote wanaokumbana na changamoto za kisheria, hususan wafanyakazi wa ndani, wafanyabiashara wadogo, na watu wanaodhulumiwa haki zao za msingi.
Wananchi wanahimizwa kujitokeza ili kupata ushauri na msaada wa kisheria unaotolewa bure kupitia kampeni hii, ambayo imekuwa msaada mkubwa kwa wananchi wanaokumbana na changamoto za kisheria na unyanyasaji wa aina mbalimbali.