
Na Neema Kandoro,Magu
WADAU wa sekta ya elimu wilayani Magu Mkoani Mwanza wamevutiwa na juhudi za walimu kwenye shule za sekondari kwa kuweka mikakati ya kuwezesha wanafunzi kidato cha nne kutokupata alama sufuri katika masomo yao.
Mkuu wa wilaya ya Magu Rachel Kasanda alisema hayo jana wilayani humo katika hafla ya kuwapongeza walimu wa shule za sekondari kwa kufanikiwa kuondosha daraja sufuri na kupunguza ufaulu wa daraja la nne baada ya wengi kupata daraja la kwanza,pili na tatu.
Kasanda alisema kutokana na serikali ya awamu ya sita kuendelea kuongeza miundombinu mashuleni, kuongeza walimu na kuondoa karo juhudi kubwa wilayani hapo ni kutaka kuona kuwa daraja sufuri na la nne wanaondoa.
Alisema wamekubaliana na walimu wa shule za serikali na binafsi kuhakikisha kuwa wanaweka juhudi kubwa za kufundisha ili wanafunzi wasiweze kupata ufaulu wa daraja la nne na sufuri.
“Mpaka sasa wilayani kwetu tumeondoa daraja la nne na sufuri kwa asilimia zaidi ya 95” alisema Kasanda.
Mkurugenzi wilayani humo Felica Myovella alisema kuwa serikali imeendelea kutoa fedha nyingi kwa ajili ya kusaidia sekta elimu ambapo mwaka huu zaidi ya bilioni 3.3 zimewezesha kuongeza miundombunu ya madarasa, ofisi na vyoo hivyo juhudi hizo tumeelekeza ziende sambamba na kupandisha ufaulu wa wanafunzi.
Alisema wamevutiwa na matokeo ya kidato cha nne ambapo hakuna wanafunzi waliopata sufuri kwenye matokeo yao hivyo aliwasisitiza walimu hao kuendelea kuweka juhudi na kuwashirikisha wazazi ili wafanikishe malengo yao.
Meneja Mahusiano wa benki ya CRDB Kanda ya Ziwa Joyce Maluba alisema katika kuunga mkono juhudi hizo zinazofanywa na serikali kwenye sekta hiyo ya elimu taasisi yao itachangia madawati 130 kwenye shule msingi wilayani hapo.
“Benki yetu kwa kuona namna Rais wetu Dk Samia Suluhu Hassan alivyoongeza miundombinu mingi kupitia fedha za kutokomeza korona nasi tunamuunga mkono kwa kuchangia” alisema Maluba.
Alisema ujenzi mkubwa unaofanywa na serikali katika kuongeza miundombinu mashuleni kunahitaji wadau mbalimbali kuunga mkono jitihada hizo.








