Home Kitaifa KWAGWILA AWAONYA WAKURUGENZI, SERIKALI HAITAWAVUMILIA WASIO WAADILIFU

KWAGWILA AWAONYA WAKURUGENZI, SERIKALI HAITAWAVUMILIA WASIO WAADILIFU

Naibu Waziri wa Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Reuben Kwagwila, ametoa onyo kali kwa Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini dhidi ya vitendo vya kutokuwa waadilifu katika usimamizi wa miradi ya Serikali.

Akizungumza mara baada ya kusomewa taarifa na kukagua mradi wa Shule ya Amali Chikota iliyopo katika Halmashauri ya Mji Nanyamba mkoani Mtwara, amesema Rais Samia Suluhu Hassan amepeleka fedha katika maeneo mbalimbali ili wananchi wanufaike, lakini wapo wachache wanaopindisha matumizi ya fedha hizo na kuwakosesha wananchi huduma.

Naibu Waziri amesema Serikali haitakubali Rais Samia apate lawama kutokana na vitendo vya baadhi ya watendaji wasio waadilifu, huku akisisitiza kuwa hatua zitachukuliwa dhidi yao kwa niaba ya Rais.

Ninatoa wito kwa Wakurugenzi wote Tanzania nzima kufuatilia miradi ambayo Mheshimiwa Rais amepeleka fedha ili wananchi wanufaike. Kuna watu wachache wasio waadilifu wanaopindisha ili wananchi wasipate huduma, na hao tutawashughulikia. Hatutokubali Mheshimiwa Rais apate lawama kwa kazi kubwa iliyotujengea heshima kwa Watanzania,” amesema Kwagwila.

Ameongeza kuwa Wakurugenzi wote waliochukua fedha za miradi wanapaswa kuzirejesha kabla hajafika katika Halmashauri husika, akisema maeneo yote ambayo fedha za Serikali hazikutumika vizuri, wahusika wote watachukuliwa hatua ikiwemo kusimamishwa kazi. Pia amesema kuwa Desemba 2025 Serikali inatarajia kuajiri walimu elfu 7,000.

Katika hatua nyingine, Naibu Waziri ameipongeza Halmashauri ya Mji Nanyamba kwa usimamizi mzuri wa miradi ya elimu ikiwemo Shule ya Sekondari ya Amali Chikota iliyopokea zaidi ya shilingi milioni 560 na Shule mpya ya Mkondo Mmoja Njengwa iliyogharimu shilingi milioni 314.

Kwa upande wao, wazazi wamepongeza utekelezaji wa miradi hiyo. Akizungumza kwa niaba ya wazazi wenzake, Mwajabu Athumani amesema ujenzi wa Shule ya Njengwa umeondoa changamoto za miundombinu chakavu zilizokuwa zinakatisha tamaa ya wanafunzi kusoma.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!