Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji na Mbunge wa Jimbo la Ubungo Prof. Kitila Mkumbo amesema mto China ambao umekuwa changamoto kwa wakazi wa Makurumla kwa muda mrefu sasa kingo zake zinaenda kujengwa.
Akiwa ziarani katika Kata ya Makurumla Prof. Kitila amesema kingo za mto China na Gide zitajengwa kwa Mradi wa Maendeleo ya Jiji la Dar es Salaam (DMDP) kupitia Benki ya Dunia kwa urefu wa KM. 4.
“Namshukuru Sana Mhe. Rais kwa kukubali mradi wa DMDP utekelezwe katika wilaya ya Ubungo maana wilaya nyingine tayari zilishanufaika” Prof. Kitila Mkumbo.
Prof. Kitila Mkumbo amesema wakati mradi huo mkubwa ukisubiriwa wamekubaliana na Mhe. Diwani wa Makurumla Bakari Kimwanga kuwa watatenga kiasi cha Sh. Milioni 6 kutoka kwenye mfuko wa Jimbo Mwezi August kwaajili ya kupata vijana watakaosafisha mto ili kuzuia mafuriko.
Katika hatua nyingine Prof. Kitila Mkumbo ameweka wazi kuwa Zabuni ya barabara ya Midizini inayounganisha Kata za Makurumla na Manzese tayari imetangazwa wiki mbili zilizopita kwaajili ya kutafuta mkandarasi atakayetekeleza ujenzi huo utakaogharimu Sh. Bilioni 2.6.
“Barabara hii ni muhimu sana maana inaunganisha mitaa mitatu ya Kata ya Makurumla ukiwemo mtaa wa Kilimahewa, Sisi kwa Sisi, Kwa Jongo na mtaa wa Midizini kwa upande wa Kata ya Manzese” aliongeza