Tume ya Ushindani (FCC) imeanza maadhimisho ya Wiki ya Haki za Mlaji Duniani, tukio ambalo huadhimishwa kila mwaka tarehe 15 Machi. Hapa nchini, kilele cha maadhimisho hayo kitakuwa tarehe 17 Machi katika Hoteli ya Protea, Upanga, ambapo mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Viwanda na Biashara, Dkt. Selemani Jafo.
Akizungumza na waandishi wa habari leo Machi 07, 2025, jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mkuu wa FCC, William Erio, amesema kuwa wiki hii inalenga kutoa elimu kwa umma kuhusu haki za mteja, ikiwa ni pamoja na haki ya kuchagua bidhaa, haki ya kulindwa dhidi ya bidhaa hatarishi, haki ya kupata taarifa sahihi za bidhaa na huduma, pamoja na haki nyingine zinazolenga kuhakikisha mlaji analindwa dhidi ya udanganyifu na unyonyaji wa kibiashara.

Aidha, Katika kuadhimisha wiki hii, FCC imeandaa programu mbalimbali za utoaji elimu kwa wadau, wakiwemo wanafunzi wa vyuo vikuu, wafanyabiashara, na wananchi kwa ujumla. Pia, kutakuwa na kliniki maalum kwa ajili ya kutoa msaada wa kisheria kwa wateja wanaokumbana na changamoto katika soko.
Aidha, Erio amesisitiza kuwa FCC inatambua umuhimu wa usawa wa kijinsia, jambo ambalo limezingatiwa katika kaulimbiu ya mwaka huu, “Haki na Maisha Endelevu kwa Mlaji.” Kaulimbiu hii pia inahimiza matumizi ya nishati safi ya kupikia kama sehemu ya kuhakikisha inapunguza uchafuzi wa mazingira na mlaji anapata bidhaa na huduma bora zinazomlinda kiafya na kimazingira.

Pia Kwa kutambua umuhimu wa Siku ya Wanawake Duniani, FCC imeandaa zoezi maalum la upimaji wa saratani ya matiti na shingo ya kizazi kwa wanawake, ikiwa ni sehemu ya jitihada za mamlaka hiyo katika kuhakikisha afya na ustawi wa jamii.
Erio pia ametumia fursa hii kuwatakia heri waumini wa dini ya Kiislamu na Wakristo katika mfungo wa mwezi mtukufu wa Ramadhan na Kwaresima, akiwataka waendelee kumuomba Mwenyezi Mungu aijalie nchi amani na kuwaongoza viongozi wake.
Pia amewahimiza wadau wa FCC na wananchi kwa ujumla wanahimizwa kutembelea ofisi za mamlaka hiyo kupata elimu zaidi kuhusu haki zao na namna wanavyoweza kuzitetea.

Naye Mkurugenzi wa Udhibiti wa Mienendo ya Biashara Inayokatazwa kwa Mujibu wa Sheria ya Ushindani, Magdalena Utou, amesema kuwa moja ya malengo makuu ya wiki hii ni kuwajengea wananchi uelewa kuhusu haki zao na wajibu wao katika soko.

Naye Meneja Miradi wa FCS, Charles Kainkwa, amesema kuwa taasisi yake inatambua umuhimu wa haki za mlaji, hivyo inaendelea kushirikiana na FCC ili kufanikisha shughuli hizi chini ya TradeMark Africa. Ushirikiano huu unalenga kuhakikisha elimu kuhusu haki za mlaji inawafikia wananchi wengi zaidi na kuwawezesha kufanya maamuzi sahihi wanaponunua bidhaa.