Home Biashara BALOZI SALUM AWATAKA WANAFUNZI KUTOKATA TAMAA, KUPAMBANA KUFIKIA NDOTO ZAO

BALOZI SALUM AWATAKA WANAFUNZI KUTOKATA TAMAA, KUPAMBANA KUFIKIA NDOTO ZAO

Celebrating 25 Years of NHIF

📌Awasisitiza kuwa na malengo na kujiandaa kushika nafasi mbalimbali za uongozi nchini

📌 Mafanikio yanahitaji juhudi na uvumilivu

FAHARI AFYA

DODOMA, NOVEMBA 2, 2026.

KATIBU Mkuu wa Wizara ya Viwanda na Biashara, Balozi Waziri Rajab Salum, amewahimiza wanafunzi kuwa na malengo thabiti, kujiamini na kutokata tamaa wanapokabiliwa na changamoto katika safari ya kutimiza ndoto zao, akisisitiza umuhimu wa kujituma na kujiandaa kushika nafasi mbalimbali za uongozi nchini.

Balozi Salum ametoa wito huo leo, Novemba 2, 2026, jijini Dodoma, alipokutana na wanafunzi wa Chuo cha Biashara waliotembelea maonesho ya biashara na huduma za kliniki za biashara yanayofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jakaya Kikwete Convention Centre.

Akizungumza na wanafunzi hao wakati wa ziara yake ya kutembelea mabanda ya wajasiriamali, wafanyabiashara na taasisi mbalimbali zinazoshiriki maonesho hayo, amewasisitiza kutambua uwezo walionao, kujiamini na kuutumia ipasavyo katika kujenga mustakabali wao.

Amesema mafanikio yanahitaji juhudi, uvumilivu na dhamira ya dhati, hivyo vijana hawapaswi kuruhusu changamoto zinazowakabili kuwakatisha tamaa, bali wanapaswa kupambana kwa bidii ili kufikia malengo yao na kuwa sehemu ya uongozi katika sekta mbalimbali za maendeleo ya taifa.

Aidha, amewahimiza wanafunzi kutumia fursa ya kutembelea maonesho hayo kujifunza kuhusu biashara, ujasiriamali na huduma zinazotolewa na taasisi mbalimbali, ili kuongeza maarifa na uelewa utakaowawezesha kutambua na kutumia fursa zilizopo katika sekta ya viwanda na biashara.

Katika ziara hiyo, Balozi Salum alitembelea mabanda mbalimbali yaliyowakutanisha wajasiriamali, wafanyabiashara na taasisi zinazotoa huduma za kukuza biashara na ujasiriamali.

Maonesho hayo ni sehemu ya shughuli zinazoambatana na uzinduzi wa Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda ya Mwaka 2025 na Sera ya Maendeleo ya Jasiriamali Ndogo na za Kati (Toleo la 2025), zinazolenga kuimarisha maendeleo ya viwanda, kukuza ujasiriamali na kuweka mazingira bora ya ukuaji wa biashara nchini.

Maonesho hayo yanatarajiwa kuzinduliwa rasmi na Waziri wa Viwanda na Biashara, Mhe. Judith Kapinga, huku uzinduzi rasmi wa sera hizo mbili ukitarajiwa kufanyika Novemba 4, 2026, jijini Dodoma, ambapo Waziri Mkuu, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, anatarajiwa kuwa Mgeni Rasmi.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here
Captcha verification failed!
CAPTCHA user score failed. Please contact us!